Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, leo tarehe 22 Septemba 2026, amemuapisha Mhe. Othman Masoud Othman kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, katika hafla iliyofanyika Ikulu Zanzibar.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Dkt. Mwinyi amesema maridhiano yaliyofikiwa kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ACT Wazalendo ni mwanzo wa hatua mpya ya kuimarisha amani, umoja na utulivu, huku nguvu zikielekezwa zaidi katika kuharakisha maendeleo na kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi.

Halikadhalika, Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa kuapishwa kwa Mhe. Othman Masoud Othman ni hatua muhimu katika utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa kati ya CCM na ACT Wazalendo, kufuatia Tamko la Pamoja lililotiwa saini tarehe 09 Julai 2026 katika viwanja vya Ikulu Zanzibar.

Vilevile, Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza kuwa maridhiano si mwisho wa safari, bali ni mwanzo wa kazi, akiwataka viongozi na wananchi kuendeleza ushirikiano na kuelekeza nguvu katika kukuza uchumi, kuongeza ajira na fursa kwa vijana, kuwawezesha wanawake, kuimarisha utalii, kuendeleza Uchumi wa Buluu na kuvutia uwekezaji.

Naye Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman, amemshukuru Rais Dkt. Mwinyi kwa dhamana aliyopewa na kuahidi kutekeleza majukumu yake kwa uaminifu, akizingatia maslahi ya Zanzibar na wananchi wake.