Dar es Salaam. Tanzania imeendelea kuendana na mabadiliko ya mahitaji ya elimu kwa kuwekeza katika maboresho ya mitaala pamoja na mazingira ya kujifunzia, ikiwemo ujenzi wa shule 130 za awali.

Hatua hiyo imeelezwa katika Kongamano la Sita la African Curriculum Association Conference linalowakutanisha wataalamu wa elimu kutoka nchi 22 kujadili mustakabali wa mitaala barani Afrika.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe, amesema mabadiliko ya mitaala hayawezi kutenganishwa na uwekezaji katika mazingira bora ya kujifunzia.

Prof. Shemdoe amesema Tanzania imeendelea kuchukua hatua katika kuboresha elimu ili mwanafunzi aweze kutumia maarifa anayoyapata darasani katika maisha ya kila siku, badala ya kutegemea nadharia pekee.

Amesema ujenzi wa shule 130 za awali ni miongoni mwa hatua zinazolenga kuimarisha mazingira ya elimu na kuhakikisha maboresho ya mitaala yanaungwa mkono na miundombinu inayokidhi mahitaji ya wanafunzi.

Kwa mujibu wa Prof. Shemdoe, maboresho hayo yanahitaji ushirikiano wa taasisi mbalimbali, akizitaja Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) pamoja na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar.

Amesema ushirikiano huo unalenga kuhakikisha mabadiliko katika mitaala yanaendana na mahitaji ya jamii, maendeleo ya teknolojia na mahitaji ya soko la ajira.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Dkt. Mwanakhamisi Adam Ameir, amesema Tanzania na Zanzibar zinapata nafasi ya kujifunza kutoka mataifa mengine kuhusu namna bora ya kukabiliana na changamoto za kubadili mitaala.

Amesema mtaala unaotekelezwa tangu mwaka 2023 umeweka mkazo katika maeneo yanayohusisha teknolojia na elimu ya amali, kwa lengo la kuwajengea vijana ujuzi unaoweza kutumika katika maisha ya kila siku na kwenye soko la ajira.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania, Dkt. Aneth Komba, amesema mjadala wa kongamano hilo unalenga pia kuhimiza Afrika kuwa na mitaala inayozingatia utambulisho, historia, tamaduni na mazingira ya bara hilo.

Dkt. Komba amesema kongamano hilo la siku nne linatarajiwa kuzaa Azimio la Dar es Salaam kuhusu mitaala ya Afrika, mwongozo wa uundaji wa mitaala pamoja na mapendekezo ya utekelezaji, huku washiriki wakitarajiwa kutembelea shule siku ya mwisho kuona kwa vitendo utekelezaji wa maboresho ya elimu.