Arusha
Wataalamu kutoka Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini cha Wizara ya Nishati, wakiongozwa na Mkurugenzi wa Kitengo hicho, Bi. Anitha Ishengoma, wameshiriki katika Kongamano la Tano la Kitaifa la Ufuatiliaji, Tathmini (5th Tanzania Monitoring, Evaluation and Learning – MEL Conference 2026) linalofanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 22 hadi 26 Septemba 2026.
Kongamano hilo linafanyika chini ya kaulimbiu “From Evidence to Action: Strengthening Human-Centered Evaluation for Sustainable Development”, inayosisitiza umuhimu wa kutumia ushahidi na matokeo ya tathmini katika kuchochea hatua madhubuti za maendeleo endelevu zinazomweka mwananchi kuwa kiini cha maendeleo.
Kongamano hilo linawakutanisha watendaji wa Serikali, wataalamu wa ufuatiliaji na tathmini, watafiti, washirika wa maendeleo pamoja na wadau mbalimbali, kwa lengo la kubadilishana uzoefu, maarifa na mbinu bora katika matumizi ya takwimu, ushahidi na matokeo ya tathmini katika uandaaji na utekelezaji wa sera, mipango na miradi ya maendeleo.
Katika kipindi cha siku tano, washiriki wanapata fursa ya kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu mifumo madhubuti ya ufuatiliaji na tathmini, matumizi ya takwimu na ushahidi katika kufanya maamuzi, pamoja na namna matokeo ya tathmini yanavyoweza kutumika kuboresha utekelezaji wa mipango, programu na miradi, na hatimaye kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Ushiriki wa Wizara ya Nishati katika kongamano hilo ni sehemu ya jitihada za kuimarisha matumizi ya takwimu, ushahidi na matokeo ya tathmini katika kufuatilia utekelezaji wa mipango, programu na miradi ya sekta ya nishati.
Aidha, ushiriki huo unalenga kuendelea kuimarisha utamaduni wa kufanya maamuzi yanayotegemea ushahidi (evidence-based decision making) na kuhakikisha matokeo ya ufuatiliaji na tathmini yanatumika ipasavyo katika kuboresha utendaji na utekelezaji wa mipango ya sekta ya nishati, sambamba na kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

