Mhe. Dkt Jakaya Mrisho Kikwete, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ameshiriki katika Mkutano wa Jopo la Kimataifa la Ngazi ya Juu kuhusu Uwekezaji katika Sekta ya Maji barani Afrika na Ushirikiano wa Kimataifa, uliofanyika pembezoni mwa Kikao cha 81 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.

Katika mkutano huo, Dkt Kikwete, akiwa Mwenyekiti Mwenza Mbadala wa Jopo hilo, aliwasilisha Ripoti ya Maendeleo ya Mpango wa Uwekezaji katika Sekta ya Maji barani Afrika (AIP), pamoja na Jedwali la Viashiria vya Uwekezaji wa AIP katika Sekta ya Maji.

Ripoti hiyo imeonesha maendeleo yaliyofikiwa, mafanikio yaliyojitokeza, changamoto zilizopo na njia za kuharakisha uwekezaji katika sekta ya maji barani Afrika, kwa lengo la kuhakikisha huduma salama na endelevu za maji zinawafikia wananchi wengi zaidi.

Mkutano huo uliwakutanisha Wakuu wa Nchi na Serikali, viongozi wa mashirika ya kimataifa, taasisi za fedha za maendeleo na washirika wengine wa kimkakati. 

Uliongozwa na Mhe. Dkt Netumbo Nandi-Ndaitwah, Rais wa Jamhuri ya Namibia na Mwenyekiti Mwenza wa Jopo la Kimataifa la Ngazi ya Juu kuhusu Uwekezaji katika Sekta ya Maji barani Afrika.