Kamati ya Bunge inayoshughulikia Masuala ya Kikanda na Utatuzi wa Migogoro katika Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) Septemba 22, 2026 imekutana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, jijini Dodoma, kwa lengo la kutathmini hatua iliyofikiwa na Tanzania katika mchakato wa ukusanyaji wa maoni ya wananchi kuhusu Rasimu ya Katiba ya Fungamano la Kisiasa la Afrika Mashariki.

Kikao hicho, kiliongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Maina Karobia, huku Ujumbe wa Wizara ukiongozwa na Mkurugenzi Idara ya Siasa, ulinzi na Usalama Bi. Mwanamridu Amiry. Wajumbe walipokea taarifa kuhusu mchakato huo na kutathmini namna wananchi wa Tanzania watakavyoshirikishwa katika kutoa maoni na mitazamo yao kuhusu Rasimu ya Katiba ya Fungamano la Kisiasa.

Tathmini hiyo ni sehemu ya juhudi za kikanda za kuhakikisha mchakato wa kuanzishwa kwa Rasimu ya Katiba ya Fungamano la Kisiasa unakuwa wa wazi, shirikishi na unaozingatia maoni na matakwa ya wananchi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.  

Kamati pia ililenga kubaini mafanikio yaliyopatikana, changamoto zilizojitokeza na maeneo yanayohitaji maboresho kabla ya kuanza mchakato huo.