Na Mwandishi Maalumu – Dodoma
21/09/2026 Kwa mara ya kwanza huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo zimeanza kutolewa ndani ya treni ambapo wasafiri wanaotumia treni ya mwendokasi (SGR) ufanyiwa uchunguzi wa magonjwa hayo wakati wa safari.
Huduma hiyo inatolewa kupitia kambi maalumu ya siku saba inayofanywa na Wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Shirika la Reli Tanzania (TRC) ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha siku ya moyo duniani ambayo uadhimishwa kila ifikapo tarehe 29 mwezi Septemba.
Akizungumza wakati wa kambi hiyo daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Samweli Msigwa alisema huduma hizo zinatolewa kwa abiria wanaosafiri na treni ya SGR ikiwa ni sehemu ya kuisogozea jamii huduma za kibingwa karibu.
Dkt. Samweli alisema jamii imekuwa ikitumia muda mwingi kufanya shughuli mbalimbali na kukosa muda wa kupima afya zao lakini kupitia kambi hiyo abiria wa SGR wamejitokeza kwa wingi kufanya uchunguzi wa afya.
“Tumeanza kuona mafanikio ya kambi hii mapema leo ikiwa ni siku ya kwanza, abiria wanaosafiri na Treni ya SGR wamefurahishwa na uwepo wetu, wamejitokeza kwa wingi kupima afya zao na hii inaonesha kuwa uhitaji ni mkubwa”, alisema Dkt. Samweli
Kwa upande wao abiria wanaosafiri na Treni ya SGR wameishukuru Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuona umuhimu wa kuwafikishia huduma hizo wakati wa safari kwani ni kweli kutokana na shughuli mbalimbali za maisha wamekuwa wakishindwa kufika hospitali kwaajili ya kufanya uchunguzi wa afya.
Mwifadhi Mrisho akiwa katika treni hiyo kuelekea Mkoani Morogoro alisema huduma za uchunguzi wa afya ni za nadra hivyo zinapojitokeza ni fursa kwa jamii kujua afya zao, kupata elimu ya namna ya kujikinga na magonjwa mbalimbali yakiwemo magonjwa ya moyo.
“Natamani zoezi hili liwe endelevu kila tukipanda treni tukutane na huduma za uchunguzi wa afya kwani mnatusaidia sana na kuokoa maisha yetu”, alisema Mwifadhi
Mwifadhi alisema huduma hizo angeenda kuzipata hospitalini angetumia muda mwingi na gharama kubwa lakini kupitia kambi hiyo amefanyiwa vipimo vya moyo bila gharama.
Naye Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Mpwapwa Luzineth Kingamkoni ameuomba uongozi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuweka huduma za uchunguzi wa matibabu ya moyo katika treni zake zote ili kila mwananchi afikiwe na huduma hizo.
“Nawaomba wasafiri wenzangu wawe tayari kupima afya zao kwani wataalamu wanatoa huduma bora, rahisi, na inatuwezesha kukagua afya zetu na kuwa salama”, alisema Askofu Luzineth

