Na Mwandishi wetu, Ngorongoro

Hayawi hayawi sasa yamekuwa, tarehe 22 Septemba, 2026 wahifadhi Duniani kote wanaungana kuadhimisha siku ya Faru ambapo Hifadhi ya Ngorongoro inaadhimisha siku hii huku ikikumbuka jinsi faru Vicky alivyomchanganya faru Telele mpaka akamwacha faru John.

Faru Vicky alikuwa na mahusiano na faru John, lakini tabia ya faru John ilikuwa ni ukorofi uliopitiliza na hasa kupigana na madume ya faru wenzie na kujipa utawala wa majike mengi.

Siku moja faru Vicky akiwa na faru Telele alitokea faru John na kuanzisha vurugu za kumpiga faru Telele, hata hivyo faru Telele hakutaka kupambana na faru John alitulia kimya kama maji ya mtungini.

Baada ya vurugu hizo faru Telele aliamua kuondoka eneo la tukio na kumuacha faru Vicky akiwa na na faru John, kwa bahati mbaya faru John akapitiwa na usingizi.

Faru Vicky alipoona faru John amelala hoi alimtoroka na kwenda kwa Faru Telele na kisha kuanzisha mahusiano na huo ndiyo ulikuwa mwisho wa enzi kwa uhusiano wa faru Vicky na faru John.

Faru Telele anapendwa na majike ya faru kutokana na utulivu na upole wake kwani yeye kwenye mahusiano hatumii nguvu zaidi ya nyama ya ulimi, kubembeleza, kudekeza na upole wake.

Matukio ya kuvutia kama haya ndiyo yaliwavutia wageni wakiwemo wanafunzi wa shule ya sekondari Embaraway iliyopo ndani ya hifadhi ya Ngorongoro kufika hifadhi ya Ngorongoro kujifunza shughuli za uhifadhi wa Faru.

Wakiwa katika Bonde la Ngorongoro , wanafunzi hao walipata fursa ya kujionea uhifadhi wa wanyama mbalimbali na kujifunza uhifadhi wa Faru, tabia, mwenendo na umuhimu wake kiuhifadhi, elimu, utafiti na utalii.

Afisa Uhifadhi Mwandamizi na Mratibu wa Faru Ngorongoro Deogratius Maige alisema kuwa, kutoa elimu kwa jamii kuhusu uhifadhi wa faru imekuwa ni sehemu ya juhudi za Mamlaka hiyo katika kuimarisha uelewa na ushiriki wa jamii katika uhifadhi, na kuhakikisha kuwa wanajenga kizazi cha baadae cha wahifadhi bora.

Kauli mbiu ya Siku ya Faru Duniani ni “Keep the Five Alive”