Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu Zanzibar, Dkt. Saada Mkuya, akizungumza kwa niaba ya Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba, wakati akifungua Mkutano wa 19 wa Wataalamu wa Ukaguzi wa Ndani na Jukwaa la 13 la Utawala Bora unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC)

 

………

Na Happy Lazaro, Arusha.

Wakaguzi wa ndani wametakiwa kwenda zaidi ya kuhakiki uzingatiaji wa taratibu, kanuni na mifumo katika taasisi, badala yake kutumia taaluma yao kutoa maarifa, mtazamo wa kitaalamu na ushauri unaosaidia kuboresha utendaji, kusimamia vihatarishi na kufikia malengo ya taasisi.

Hayo yamesemwa leo jijini Arusha na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu Zanzibar, Dkt. Saada Mkuya, kwa niaba ya Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba, wakati akifungua Mkutano wa 19 wa Wataalamu wa Ukaguzi wa Ndani na Jukwaa la 13 la Utawala Bora unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC).

Dkt. Mkuya amesema kupitia kaulimbiu ya “Beyond Assurance, Driving Insight, Driving Innovation,” wakaguzi wanapaswa kuhakikisha taarifa wanazozalisha zinatumika katika kufanya maamuzi na si kuishia kusomwa wakati wa vikao.

Amesema taarifa sahihi, za kuaminika na zisizo na upendeleo ni msingi wa maamuzi bora, hasa katika mazingira yanayobadilishwa na teknolojia, mabadiliko ya kiuchumi na vihatarishi vipya.

Dkt.Mkuya amesema kuwa, maendeleo ya teknolojia na matumizi ya akili bandia yamefanya ubunifu kuwa hitaji la kimkakati, hivyo taasisi zinapaswa kujiandaa kukabiliana na changamoto za siku zijazo kwa kuboresha mifumo na namna ya kufanya kazi.

Kwa msingi huo, wakaguzi wametakiwa kushiriki katika kuchochea maboresho na ubunifu huku wakizingatia misingi ya utawala bora.

Aidha, amewataka wakaguzi kuendelea kujiendeleza kitaaluma, kufanya tafiti na kuongeza maarifa ili kuendana na mabadiliko ya mazingira ya kazi.

Ameongeza kuwa, utekelezaji wa Global Internal Audit Standards ni muhimu katika kuimarisha ubora, weledi na uaminifu wa taaluma hiyo katika sekta ya umma na binafsi.

“Uaminifu ni rasilimali muhimu kwa taasisi kwa kuwa hujenga imani ya wananchi na kuongeza utayari wao wa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu.”amesema .

Amewataka wakaguzi kujivunia taaluma yao, kusimamia ukweli na kutoa ushauri huru wa kitaalamu hata pale ambapo maoni yao yanaweza kutokubalika kwa baadhi ya viongozi au watendaji.

Aidha amewataka kuwekeza katika mafunzo ya mara kwa mara ili kuwajengea uwezo wakaguzi kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji mapya ya taaluma.

Aidha ameongeza kuwa,wakaguzi wanapaswa kuwa mabalozi wa matumizi yenye tija na kuzingatia thamani ya fedha katika matumizi ya rasilimali za umma, kwa kuwa usimamizi bora wa rasilimali unaongeza uwezo wa Serikali kuboresha huduma za afya, elimu, kilimo na miundombinu.

Aidha, Serikali imesisitiza umuhimu wa kuimarisha ukaguzi katika mamlaka za Serikali za Mitaa kama nyenzo ya kuongeza uwajibikaji na usimamizi wa fedha, sambamba na utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.

Mwenyekiti wa Mkutano wa IIA Tanzania, Dkt. Benedicto Baragomwa, amesema taasisi za Serikali na sekta binafsi zinapaswa kutumia ukaguzi wa ndani kuongeza tija, ubunifu na ufanisi wa huduma kwa wananchi, huku akieleza kuwa mkutano huo unatoa fursa kwa viongozi na wataalamu kubadilishana uzoefu kuhusu uimarishaji wa mifumo ya taasisi.

Kwa upande wake, Rais wa Taasisi ya Wakaguzi wa Ndani Tanzania (IIA Tanzania), Jonathan Ngoma, amesema kuna haja ya kuimarisha uhuru wa wakaguzi ili waweze kutoa taarifa za kitaalamu bila kuingiliwa na kuhakikisha mapendekezo yao yanafanyiwa kazi.

Amesema mabadiliko ya teknolojia yamepanua wigo wa taaluma hiyo, ambapo wakaguzi sasa wanahusika pia na teknolojia, usalama wa mitandao, vihatarishi na mifumo ya udhibiti wa ndani, badala ya kuhusisha majukumu yao na fedha pekee.