Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limemteua mwanamuziki, mtunzi wa nyimbo na mtetezi wa vijana, Abigail Chams, kuwa Balozi wake mpya wa Taifa nchini Tanzania, akitarajiwa kutumia sauti na jukwaa lake kuhamasisha haki za watoto na ustawi wa vijana balehe.

Tangazo la uteuzi huo limetolewa leo Septemba 21, 2026, katika Ofisi za UNICEF Tanzania jijini Dar es Salaam, wakati wa utekelezaji wa mpango wa kila mwaka wa Girls Take Over unaofanyika kuelekea Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike.

Akizungumza katika tukio hilo, Mwakilishi wa UNICEF nchini Tanzania, Elke Wisch, amesema uteuzi huo unaendana na umuhimu wa kuwawezesha wasichana kushiriki katika nafasi za uongozi na kutumia sauti zao katika kuleta mabadiliko chanya katika jamii.

“Leo, wakati Kuruthum anapochukua nafasi yangu na kushirikisha maono yake kuhusu mustakabali wa Tanzania, tunaona umuhimu wa kuunda fursa kwa wasichana kushiriki katika nafasi za uongozi,” amesema Wisch.

Amesema mpango huo pia unatoa fursa kwa wasichana kukutana na watu wanaowaangalia kama mfano wa kuigwa na kujifunza kutokana na uzoefu wao, akieleza kuwa Abigail ana uzoefu, ubunifu na ushawishi katika kutetea masuala yanayowahusu vijana.

“Abigail anakuja na uzoefu wake, ubunifu na ushawishi wake katika kutetea masuala ya vijana, na tunafurahia kumpokea kama Balozi wa Taifa wa UNICEF. Tunatumaini kuwa mfano wake utawatia moyo wasichana wengi zaidi kujiona kuwa viongozi, kutumia sauti zao na kuamini katika kile kinachowezekana,” amesema.

Abigail amewahi kushirikiana na UNICEF kama Mtetezi wa Vijana, akitumia jukwaa lake kuhamasisha haki za wasichana, ustawi wa afya ya akili na mabadiliko chanya katika jamii.

Katika nafasi yake mpya, Abigail atatumia ushawishi wake kuunga mkono uhamasishaji kuhusu afya ya akili, ulinzi wa watoto, kukomesha ukatili dhidi ya watoto na kuwawezesha vijana balehe.

Aidha, Abigail na UNICEF wamezindua kampeni mpya ya ‘Hauko Solo’ inayolenga kuwahamasisha vijana kuzungumza kwa uwazi kuhusu hisia zao, kutafuta msaada na kufahamu kuwa hawako peke yao, huku akihamasisha matumizi ya Mstari wa Msaada kwa Watoto 116.

Kampeni hiyo imekuja baada ya Abigail kufanya ziara katika kituo cha Mstari wa Msaada kwa Watoto kinachoendeshwa na C-Sema, ambapo alikutana na vijana, wazazi na walezi na kujifunza zaidi kuhusu huduma zinazotolewa kupitia namba 116.

Katika tukio hilo, Kuruthum Massiro kutoka Mkoa wa Mwanza alichukua nafasi ya Mwakilishi wa UNICEF kwa siku moja kupitia mpango wa Girls Take Over, akipata fursa ya kushiriki katika majukumu ya uongozi na kukutana na Abigail Chams.

Mpango wa Girls Take Over unaotekelezwa kwa ushirikiano na Plan International unawapa wasichana fursa ya kushiriki katika nafasi za uongozi na kutoa mitazamo yao kuhusu masuala yanayoathiri maisha yao, huku kaulimbiu ya mwaka huu ikiwa ni “Komesha Ndoa za Utotoni na Wekeza katika Haki za Wasichana.”