Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umetoa mafunzo kwa viongozi wa Serikali za Mitaa pamoja na wajasiriamali katika Halmashauri za Mkoa wa Lindi, kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kuhamasisha matumizi ya nishati ya umeme yenye tija kiuchumi pamoja na nishati safi ya kupikia.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi MKuu wa REA, Afisa Maendeleo ya Jamii Mwandamizi kutoka REA, Bi. Jaina Msuya, amesema mafunzo hayo yanayofanyika katika wilaya mbalimbali za Mkoa wa Lindi yanalenga kuwaongezea washiriki uelewa na ujuzi wa namna ya kuelimisha na kuhamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa matumizi ya umeme yenye tija kiuchumi na kutumia nishati safi ya kupikia.

Amesema mafunzo hayo pia yanahusu matumizi ya umeme katika shughuli za uzalishaji, ikiwa ni pamoja na kuwasaidia wananchi kutumia fursa zinazotokana na mnyororo wa miradi ya kusambaza nishati vijijini ili waweze kutambua fursa na kuzitumia kukuza shughuli zao za kiuchumi na kuboresha ustawi wa jamii.

Kwa mujibu wa Bi. Msuya, Maafisa Maendeleo ya Jamii pamoja na Watendaji wa Kata wana nafasi muhimu katika kuwa mabalozi wa matumizi ya nishati safi ya kupikia na matumizi yenye tija ya umeme kwa shughuli za uzalishaji, kwa kuwa wanafanya kazi moja kwa moja na wananchi katika maeneo mbalimbali.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Benki ya CRDB amewahimiza wananchi na wajasiriamali kuchangamkia fursa za mikopo zinazotolewa na benki hiyo ili kuwekeza katika miradi ya kusambaza nishati vijijini kwa kuanzisha viwanda vidogo vya kusindika mazao ya kilimo, ufugaji na uvuvi pamoja na kuanzisha biashara ndogo ndogo.

Amesema uwekezaji katika nishati safi ya kupikia una fursa za kiuchumi kwa wananchi, huku ukichangia kupunguza matumizi ya nishati zisizo safi na salama kwa mazingira.

Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za REA za kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu matumizi bora ya nishati, kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia pamoja na kuhamasisha matumizi ya umeme katika shughuli za uzalishaji mali katika Mkoa wa Lindi.