Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imetoa mafunzo ya usimamizi wa mikataba ya ujenzi kupitia Mfumo wa NeST kwa watumishi wa umma, Septemba 14 – 18, 2026, jijini Arusha.

Meneja wa Kuendeleza Uwezo na Huduma za Ushauri, Bw. Gilbert Kamnde, amesema Mamlaka hiyo imetoa mafunzo hayo kwa wasimamizi wa mikataba na wataalamu wa ununuzi kutokana na kuanza kutumika kwa moduli mpya katika Mfumo huo.

Ameeleza kuwa mafunzo hayo yametolewa kwa ajili ya kuhakikisha kuwa usimamizi wa mikataba unafanyika kwa ufanisi kupitia Mfumo wa NeST na kwamba kila hatua ya utekelezaji wa mkataba, hadi kufikia malipo, inarekodiwa ipasavyo ili kurahisisha taratibu za ukaguzi na kuongeza uwajibikaji.

Aidha, amesema Mamlaka hiyo inaendelea kutoa mafunzo kwa watumishi wa umma ili kuwajengea uwezo wa kutumia Mfumo wa NeST katika utekelezaji wa michakato ya ununuzi wa umma. Amesema PPRA pia imeandaa mafunzo kwa waajiriwa wapya Serikalini, yatakayofanyika Septemba 28 – Oktoba 9, 2026, mjini Morogoro.

“Mafunzo yatakayofanyika Septemba 28 – Oktoba 9, 2026, mjini Morogoro yatakuwa mafunzo ya msingi kuhusu matumizi ya Mfumo wa NeST na Sheria ya Ununuzi wa Umma. Watumishi wapya wa Serikali na watumishi wengine wanaohitaji kupata uelewa wa kina kuhusu masuala ya msingi, tunawaalika wajisajili sasa kupitia tsms.ppra.go.tz,” amesema Bw. Kamnde.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo, Bw. Emmanuel Ng’oina, Mhandisi Mjenzi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, amesema kutokana na mafunzo waliyopata, usimamizi wa mikataba kupitia Mfumo wa NeST utakuwa wa haraka na wenye uwazi zaidi, pamoja na kuongeza uwajibikaji.

PPRA inaendelea kutoa mafunzo kuhusu Mfumo wa NeST na Sheria ya Ununuzi wa Umma, ambapo wiki hii inaendelea kutoa mafunzo kwa kundi lingine jijini Arusha. Kalenda ya mafunzo ya NeST inapatikana katika tovuti ya PPRA.