Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo amefungua Mkutano wa Pili wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Vietnam unaofanyika jijini Dar es Salaam Septemba 21 hadi 23, 2026.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo Septemba 21, 2026, Balozi Dkt. Shelukindo amesisitiza umuhimu wa kuendeleza uhusiano wa kihistoria na wa kirafiki uliopo kati ya Tanzania na Vietnam, pamoja na kutumia fursa zilizopo katika kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Amesema kwa muda mrefu, uhusiano baina ya nchi hizi mbili umeendelea kukua na kuimarika katika maeneo yenye manufaa kwa pande zote mbili, hususan katika biashara na uwekezaji, kilimo, miundombinu, teknolojia, mawasiliano, ulinzi na usalama na sekta nyingine za maendeleo.
Pia ameeleza kuridhishwa na ukuaji wa sekta ya biashara na uwekezaji kati ya nchi hizi mbili katika miaka ya hivi karibuni. “Ukuaji wa biashara kati ya nchi hizi mbili umeongezeka kutoka Dola za Marekani Milioni 248.4 mwaka 2020 hadi Dola za Marekani Milioni 368.2 mwaka 2025. Vietnam ni mnunuzi wa pili duniani wa Korosho ya Tanzania na mnunuzi wa tatu mkubwa duniani wa Pamba ya Tanzania” amesema Katibu Mkuu.
Kuhusu uwekezaji, amesema eneo hilo pia limeendelea kuimarika ambapo kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Vietnam, Kampuni ya Simu ya Halotel kutoka Vietnam imewekeza zaidi ya Dola za Marekani Bilioni moja hapa nchini ikiwa na watumiaji wa mtandao huo zaidi ya milioni 16 na kutengeneza ajira zaidi ya 20,000.
Kwa upande wake, kiongozi wa ujumbe wa Vietnam kwenye Mkutano huo, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa wa Wizara ya Kilimo ya Vietnam, Bw. Pham Ngoc Mau amesema nchi hiyo inathamini uhusiano wake na Tanzania na ipo tayari kushirikiana katika kutekeleza maeneo ya makubaliano yatakayofikiwa katika mkutano huo.
Mkutano huo utahitimishwa tarehe 23 Sepemba 2026 kwa kikao cha ngazi ya Mawaziri.

