Dodoma, Septemba 19, 2026
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, amezindua Kampeni ya Usafi Endelevu ya Mkoa yenye kaulimbiu “Dodoma Fahari Yetu, Usafi ni Wajibu Wetu”, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha miji nchini inaendelea kuwa safi na salama.
Akizindua kampeni hiyo leo, Septemba 19, 2026, katika maadhimisho ya Siku ya Usafi Duniani yaliyofanyika Kata ya Msalato, Jijini Dodoma, Mhe. Senyamule amesema usafi si jambo la hiari, bali ni wajibu wa kila mwananchi na taasisi.
“Suala la usafi ni wajibu wa kila mtu. Uthibitisho wa usafi wetu unaonekana kupitia mazingira yetu. Usafi si dhamira ya mtu binafsi pekee, bali ni wajibu wa kila mmoja, kwa sababu usafi ni afya, heshima na nidhamu,” amesema Mhe. Senyamule.
Mhe. Senyamule amesisitiza kuwa, pamoja na uzinduzi wa kampeni hiyo endelevu, wananchi wanapaswa kuendelea kushiriki kufanya usafi kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi, huku siku hiyo ikitumika pia kufanya ukaguzi wa usafi katika maeneo mbalimbali bila kuathiri shughuli za kiuchumi.
Amesema mtu, taasisi au eneo litakalobainika kuwa chafu litachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria, ikiwemo kutozwa faini, akisisitiza kuwa kampeni hiyo ni mwanzo wa utekelezaji endelevu wa wajibu wa usafi na si zoezi la siku moja.
Aidha, Mhe. Senyamule amekemea utupaji holela wa mifuko na vifungashio vya plastiki unaochafua mazingira na taswira ya Dodoma kama Makao Makuu ya Nchi, akitaka kuwepo kwa utaratibu madhubuti wa ukusanyaji na urejerezwaji wa vifungashio vinavyoruhusiwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mhe. Jabir Shekimweri, amesema Halmashauri ya Jiji la Dodoma imetenga shilingi bilioni 3 kwa ajili ya shughuli za usafi, hususan ukusanyaji na utupaji taka. Aidha, amesema Halmashauri imeongeza wazabuni wa ukusanyaji taka na ina vikundi 20 vya kijamii vinavyoshiriki katika shughuli za usafi.
Akiwasilisha taarifa kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Taka na Usafi wa Mazingira, Bw. Mkana M. Mkana, amesema Jiji limefanya ukaguzi katika kaya 2,675 na biashara 1,582, ambapo jumla ya shilingi 5,660,000 zilikusanywa kama tozo kutoka kwa waliobainika kuchafua mazingira.
Amesema Jiji pia limeendelea kuwaondoa wafanyabiashara waliokuwa wakifanya biashara katika maeneo yasiyo rasmi na kuwaelekeza katika maeneo rasmi, ikiwemo masoko.
Kwa upande wao baadhi ya wakazi wa Kata ya Mnadani walioshiriki katika zoezi la usafi kama sehemu ya uzinduzi wa kampeni hiyo, wamesema usafi ni jukumu la kila mwananchi na wameahidi kuendelea kushiriki katika usafi wa mazingira kwa pamoja, ikiwemo kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi, ili kulinda afya, mazingira na hadhi ya Dodoma.
Kampeni hiyo inalenga kuimarisha ushiriki wa wananchi na taasisi katika kuhakikisha Dodoma inaendelea kuwa safi, salama na yenye hadhi inayolingana na nafasi yake kama Makao Makuu ya Nchi.

