Naibu Waziri wa Afya na Mbunge wa Jimbo la Muhambwe, Dkt. Florence Samizi, amekabidhi vifaa mbalimbali vyenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 87 katika maeneo mbalimbali ya Jimbo la Muhambwe, Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo, Mkoa wa Kigoma, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi alizozitoa wakati wa kampeni.

Vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na mabati 1,050 yenye thamani ya Shilingi milioni 37, saruji mifuko 289 yenye thamani ya Shilingi milioni 6.936, pamoja na kompyuta na printa moja vyenye thamani ya Shilingi milioni 3.5.

Aidha, Dkt. Samizi ametoa zaidi ya Shilingi milioni 40 kwa ajili ya ujenzi wa vivuli katika maeneo ya masoko, hatua inayolenga kuboresha mazingira ya wafanyabiashara na wananchi wanaotumia masoko hayo.

Dkt. Samizi amekabidhi vifaa hivyo akiwa katika ziara ya jimboni kwake, ikiwa ni sehemu ya kuendelea kuwashukuru wananchi kwa ushirikiano wao pamoja na kutekeleza ahadi alizozitoa wakati wa kampeni.

Katika ziara hiyo, Dkt. Samizi amewaasa wananchi kuendelea kutumia fursa zinazopatikana katika kilimo, ikiwemo kulima zao la parachichi, ambalo linaweza kuwa chanzo cha kipato na kuchangia katika kukuza uchumi wa kaya.

Aidha, amewataka wananchi kuchukua tahadhari na kujiandaa kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na El Niño, ikiwa ni pamoja na kufuata maelekezo yanayotolewa na mamlaka husika kuhusu hali ya hewa na maandalizi ya kukabiliana na majanga.

Dkt. Samizi amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wananchi katika kutatua changamoto zao na kuweka mazingira wezeshi ya maendeleo, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kutumia fursa zinazopatikana katika maeneo yao kwa ajili ya kujiletea maendeleo.