Dodoma, Septemba 18, 2026
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, ametoa wito kwa Taasisi za Serikali Mkoani Dodoma kuhakikisha zinawawezesha watu wenye ulemavu kujitegemea na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kijamii kwa kuwawekea mazingira rafiki na kuwawezesha kupata fursa mbalimbali za maendeleo.
Mhe. Senyamule ameyasema hayo leo, Septemba 18, 2026, wakati wa hafla fupi ya kukabidhi viti mwendo kwa watu wenye ulemavu iliyofanyika katika viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma. Viti mwendo hivyo vimetolewa na Taasisi ya ‘Human Rights and Economic Development for Disabled Persons’ (HREDP) ya Jijini Dar es Salaam, inayojishughulisha na utengenezaji wa vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu.
Amesema Serikali imeweka taratibu na mifumo mbalimbali ya kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata fursa sawa za kushiriki katika shughuli za maendeleo, hivyo ni muhimu kila Taasisi ya Serikali kutekeleza wajibu wake ipasavyo.
“Dhamira ya Serikali ni kutaka watu wenye ulemavu waishi kwa furaha, waweze kujitegemea, kufanya shughuli za kiuchumi na kumudu maisha yao. Ili waweze kufanya hivyo, wanatakiwa kuwezeshwa kwa kuwekewa mazingira mazuri. Taasisi zote za Serikali, taratibu zimewekwa; kazi yetu ni kuhakikisha tunazitekeleza. Kila mmoja akitimiza wajibu wake, watu wenye ulemavu wataweza kuishi kwa furaha, kupata fursa za kiuchumi na kufanya mambo mbalimbali ya kujitegemea,” amesema Mhe. Senyamule.
Aidha, Mhe. Senyamule amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha watoto wenye ulemavu wanapelekwa shule, ili wapate haki yao ya msingi ya elimu. Amesema Serikali imeendelea kujenga na kuboresha shule za bweni zenye mazingira rafiki kwa watoto wenye mahitaji maalum, ikiwemo kuwepo kwa wataalamu wa kuwafundisha, chakula pamoja na walezi wa kuwahudumia. Mkoa wa Dodoma una shule tatu za aina hiyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa HREDP, Bw. David Nyendo, amesema ulemavu haupaswi kuwa kikwazo kwa mtu kushiriki katika maisha ya kila siku, akieleza kuwa taasisi hiyo inalenga kupunguza vikwazo vinavyowakabili watu wenye ulemavu kupitia utengenezaji na utoaji wa vifaa saidizi.
Amesema viti mwendo vilivyotolewa pia vitasaidia kupunguza changamoto wanazokabiliana nazo wazazi, hususan kina mama, wanaopata ugumu wa kuwabeba watoto wao wenye ulemavu wanapohitaji kwenda katika maeneo mbalimbali.
Baadhi ya watu wenye ulemavu waliokabidhiwa viti mwendo hivyo wameeleza kuwa msaada huo utawarahisishia usafiri na kuwapa nafasi kubwa ya kufanya shughuli zao za kila siku kwa kujitegemea. Wamesema viti hivyo vitawasaidia kupunguza utegemezi kwa familia na walezi, huku wakieleza kuwa wanatarajia kuvitumia katika shughuli za kijamii na kiuchumi kulingana na uwezo na mazingira yao.
Taasisi ya HREDP ilianzishwa mwaka 2006, ikiwa na ofisi katika Jengo la Machinga Complex na karakana katika eneo la Chang’ombe, Jijini Dar es Salaam. Taasisi hiyo hutengeneza viti mwendo kwa kutumia vyuma chakavu vinavyotolewa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).
Katika hafla hiyo, HREDP imekabidhi viti mwendo 20 kwa Mkoa wa Dodoma vyenye thamani ya takribani shilingi milioni 5.

