Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akizungumza na waumini wa dini ya Kiislamu katika Dua Maalum ya kuliombea Taifa, kuwaombea viongozi wa nchi na kumuomba Mwenyezi Mungu kuliepusha Taifa na madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na hali ya El Niño, iliyofanyika leo, tarehe 18 Septemba 2026, katika Almadrasat Swifat Nabawiyatil Karimah, Msolopa Kilimani, Mkoa wa Mjini Magharibi.
…………….
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesisitiza umuhimu wa madrasa katika kujenga kizazi chenye elimu ya dini, maadili mema na misingi imara ya malezi, akieleza kuwa nafasi hiyo ni muhimu katika kuwaandaa watoto na vijana kukabiliana na changamoto na vishawishi vinavyojitokeza katika jamii ya sasa.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 18 Septemba 2026, katika dua maalum ya kuliombea Taifa, kuwaombea viongozi wa nchi pamoja na kumuomba Mwenyezi Mungu kuliepusha Taifa na madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na hali ya El Niño, iliyofanyika katika Almadrasat Swifat Nabawiyatil Karimah, Msolopa Kilimani, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Amesema elimu ya dini inayotolewa katika madrasa ina mchango mkubwa katika kuwajenga watoto na vijana kuwa na misingi imara ya maadili, heshima na uwajibikaji, na kuwaandaa kuwa raia wenye mchango chanya katika jamii.
Alhaj Dkt. Mwinyi amesisitiza umuhimu wa walimu wa madrasa, wazazi na walezi kushirikiana kwa karibu katika malezi ya watoto tangu wakiwa wadogo, hususan katika kipindi hiki ambacho matumizi ya teknolojia na mitandao ya kijamii yameongezeka.
Amesema mitandao ya kijamii ina manufaa mengi, ikiwemo kupata elimu na maarifa, hivyo matumizi yake yanahitaji uangalizi wa karibu ili watoto na vijana wanufaike nayo kwa njia sahihi na kuepuka taarifa au maudhui yanayoweza kuathiri malezi na mienendo yao.
Rais Dkt. Mwinyi amesema jukumu la malezi haliwezi kuachiwa upande mmoja, bali linahitaji ushirikiano wa wazazi, walezi, viongozi wa dini, taasisi za elimu pamoja na jamii kwa ujumla.
Alhaj Dkt. Mwinyi amehimiza wananchi kuendelea kudumisha umoja, mshikamano na ushirikiano, akieleza kuwa misingi hiyo ina nafasi muhimu katika kuimarisha amani, utulivu na maendeleo ya Zanzibar.
Amesema mchango wa viongozi wa dini na viongozi wengine katika kujenga maelewano miongoni mwa wananchi ni muhimu katika kuendeleza mazingira ya amani nchini.
Dkt. Mwinyi amewashukuru viongozi wa dini, viongozi wa Serikali, wananchi pamoja na wageni walioshiriki katika dua hiyo. Aidha, amehimiza wananchi kuendelea kumuomba Mwenyezi Mungu kuliepusha Taifa na madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na mvua kubwa zinazotarajiwa kunyesha, sambamba na kuchukua tahadhari na kuzingatia taarifa na maelekezo yanayotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) pamoja na Serikali.
Naye, Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Mhe. Nadir Abdullatif Alwardy, amesema katika nasaha zake kuwa kila Muislamu anapaswa kuendelea kumtii na kumuabudu Mwenyezi Mungu kwa kuzingatia mafundisho ya dini na kuyatekeleza katika maisha yake ya kila siku. Amesema kumcha Mwenyezi Mungu na kuzingatia mafundisho ya dini ni miongoni mwa misingi ya kujenga jamii yenye maadili mema, amani na mshikamano.

