Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Mussa, Septemba 18, 2026 ameungana na Balozi wa Afrika Kusini nchini Tanzania Mheshimiwa Noluthando Mayende-Mlepe, kutembelea Gereza la Segerea jijini Dar es Salaam na kufanya mazungumzo na Kamishna Msaidizi wa Magereza, Hamis Ngaukia. Ziara hiyo ni sehemu ya kuadhimisha Siku ya Hayati Nelson Mandela, inayoadhimishwa duniani kote kila ifikapo Julai 18.
Maadhimisho hayo yaliyoandaliwa na Ubalozi wa Afrika Kusini nchini Tanzania ukishirikiana na Umoja wa Mataifa Tanzania na Taasisi ya kujifunza na ujifunzaji wa Bibilia nchini Tanzania yamelenga kujenga matumaini, kuhamasisha matendo chanya, na kukuza ujumuishi wa kijamii kwa wanawake walioko gerezani. Hafla hiyo imeweka msisitizo katika kuwajenga kisaikolojia na kuwapa moyo wafungwa hao ili waweze kujiona bado ni sehemu muhimu ya jamii.
Ujumbe mkuu katika siku hiyo ulikuwa ni maisha ya baadaye ya mtu hayapaswi kuamuliwa na makosa au mazingira yake ya nyuma. Umesisitiza kuwa Maisha hayo yanaweza kubadilishwa kupitia kupata ujuzi mpya, ujasiriamali, ukarabati wa tabia, pamoja na maandalizi thabiti ya kuwezesha kurejea salama na kwa heshima katika jamii.
Vilevile katika kuyaenzi maisha na urithi wa Hayati Nelson Mandela, aliyekaa gerezani kwa miaka 27 kabla ya kuachiwa mwaka 1990, washiriki walikumbushana wajibu wa kila mtu kuleta mabadiliko chanya. Mfano wa Mandela unaendelea kuhamasisha dunia kuwa mazingira magumu ya gerezani hayapaswi kukata tamaa au kufuta ndoto za mtu.
Katika maadhimisho hayo Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Kwa Kushirikiana na Mamlaka ya Magereza, Umoja wa Mataifa, Vodacom, DHL, ARI Sanitary Pads, na Ubalozi wa Afrika Kusini wametoa Msaada wa vitu mbalimbali ikiwemo Biblia, vifaa vya usafi, taulo za kike, na magodoro kwa wanawake walioko gerezani.

