Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) imeendelea kutekeleza shughuli za uthibiti wa ubora wa mbegu nchini kwa kutembelea Mkoa wa Manyara, Wilaya ya Babati, ambapo imefanya ukaguzi katika shamba lenye ukubwa wa ekari 25 linalozalisha mbegu za vitunguu aina ya Mang’ola Red.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TOSCI, Bw. Nyasebwa Chimagu, amesema TOSCI inaendelea kushirikiana na sekta binafsi pamoja na kuwawezesha wazalishaji wa ndani ili kuongeza uzalishaji wa mbegu nchini na kupunguza utegemezi wa mbegu zinazoagizwa kutoka nje ya nchi.
Amesema Serikali inaendelea kuweka msisitizo katika uzalishaji wa mazao ya bustani, hususan mboga mboga na viungo kama vitunguu, ambayo ni miongoni mwa mazao yanayotoa fursa za kiuchumi kwa vijana na wanawake nchini. Kwa mujibu wa Bw. Chimagu, kuongeza uzalishaji wa mbegu bora ndani ya nchi kutasaidia kuimarisha upatikanaji wa mbegu kwa wakulima na kuongeza tija katika kilimo.
Aidha, Mkurugenzi Mkuu huyo amewataka wakulima kuendelea kuzingatia kanuni na taratibu za kilimo bora ili kuhakikisha wanazalisha mazao yenye tija na ubora unaokidhi mahitaji ya soko. Pia amewataka maafisa ugani kutoka NAESA kote nchini kuhakikisha wakulima wanapata elimu sahihi kuhusu mbegu bora na matumizi yake.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kanda ya Kaskazini wa TOSCI, Bw. Areth Kibaraza, amesema ofisi ya Kanda hiyo iko tayari kuwawezesha wazalishaji wa mbegu za mboga mboga kwa kuwapatia elimu na ushauri wa kitaalamu, pamoja na kuwaelekeza maeneo yanayofaa kwa ajili ya uzalishaji wa mbegu hizo.
Naye mzalishaji wa mbegu za vitunguu, Bw. Raj Shatia, ameishukuru Serikali na TOSCI kwa kuendelea kuwatambua na kuwaunga mkono wazalishaji wa mbegu nchini, akieleza kuwa ushirikiano huo unasaidia kuimarisha uzalishaji wa mbegu bora na kuchochea maendeleo ya sekta ya kilimo.

