Na Sophia Kingimali, Dar es Salaam
WATANZANIA wametakiwa kutumia changamoto za mazingira kama fursa za kukuza uchumi, kuongeza ajira na kuimarisha ustawi wa wananchi, huku ikiendelea kulinda rasilimali za asili kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Wito huo umetolewa leo Septemba 15,2026 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, mhandisi Hamad Masauni, wakati akifungua Mkutano wa Tanzania Green Summit, amesisitiza umuhimu wa kuunganisha ajenda ya mazingira na mipango ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya taifa.
Masauni amesema Tanzania iko katika hatua muhimu ya utekelezaji wa mipango yake ya maendeleo, ikiwemo Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050, hivyo ni muhimu kuhakikisha jitihada za kulinda mazingira zinaenda sambamba na kuongeza uzalishaji, ajira na fursa za kiuchumi kwa wananchi.
Amesema mazingira hayapaswi kutazamwa kama changamoto pekee, bali pia ni chanzo cha fursa zinazoweza kutumika katika teknolojia, uwekezaji, ubunifu na tafiti ili kujenga uchumi endelevu. Aliongeza kuwa shughuli zote za maendeleo zinapaswa kuzingatia uhifadhi wa rasilimali za asili ili zisihatarishe maisha ya vizazi vijavyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Grina Foundation, Redemptus Caesar, amesema taasisi hiyo imehamasika kuanzisha jukwaa hilo baada ya kuona namna mataifa mengine yanavyotumia fursa za mazingira kuvutia uwekezaji, mawazo mapya na ubunifu katika kujenga uchumi unaozingatia uhifadhi wa mazingira.
Caesar amesema Tanzania inahitaji kuongeza hamasa ya ndani katika kutumia fursa hizo, akieleza kuwa Grina Foundation inalenga pia kuwawezesha vijana kupitia programu mbalimbali zitakazowapa nafasi ya kuibua na kukuza mawazo yanayolenga kutatua changamoto za mazingira.
Ameongeza kuwa taasisi hiyo ipo tayari kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuwawezesha vijana, hususan katika ujasiriamali na ubunifu wa kimazingira, ili kuhakikisha mawazo yao yanabadilishwa kuwa fursa za kiuchumi na suluhisho zenye manufaa kwa jamii.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank, Abdulmajid Nsekela, amesema Tanzania Green Summit ni jukwaa muhimu linalowaunganisha Serikali, sekta binafsi, wawekezaji, taasisi za fedha, wabunifu, washirika wa maendeleo na jamii kwa lengo la kujenga uchumi wa kijani wenye ustahimilivu na unaotoa fursa kwa wananchi.
Nsekela amesema mjadala wa mabadiliko ya tabianchi haupaswi kuishia kwenye hasara zinazoweza kuipata Tanzania, bali unapaswa kuelekezwa kwenye thamani ya kiuchumi inayoweza kupatikana kupitia hatua za kukabiliana na mabadiliko hayo. Alitaja maeneo yenye fursa kuwa ni nishati jadidifu, kilimo himilivu kwa tabianchi, usafirishaji endelevu, ujenzi wa kijani, usimamizi wa taka, uchumi wa buluu na teknolojia safi.
Amesema sekta ya fedha ina wajibu wa kusaidia kujenga uchumi endelevu, akieleza kuwa CRDB imeendelea kutoa fedha kwa shughuli za uchumi wa kijani. Alisema benki hiyo imefanikiwa kukusanya takribani Sh bilioni 101.8 kupitia green bond, ambazo zimeelekezwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi, nishati jadidifu, nishati safi ya kupikia, usafirishaji safi, ufanisi wa matumiz
Aidha Nsekela,amesema CRDB pia imeendelea kushirikiana na wadau katika kuongeza upatikanaji wa fedha kwa miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo programu ya kukabiliana na athari za tabianchi katika kilimo ambayo imewafikia zaidi ya wanufaika 26,000 moja kwa moja na takribani 480,000 kwa njia isiyo ya moja kwa moja katika mikoa 27 nchini.
Hata hivyo Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa, Suzan Ngongi, amesema Tanzania iko katika hatua muhimu ya utekelezaji wa Dira yake ya Maendeleo, hivyo kinachohitajika sasa ni kubadili mipango na mawazo mazuri kuwa uwekezaji, biashara, miundombinu, ajira na maisha bora huku mifumo ya asili ikiendelea kuwa salama na yenye tija.
Ngongi amesema changamoto kubwa iliyopo ni namna ya kuyafikisha mawazo na ubunifu wa mazingira kwenye kiwango kikubwa, huku akisisitiza umuhimu wa kuwaunganisha wabunifu na mitaji, masoko na sera.
Alisema pia ni muhimu kuongeza idadi ya miradi inayoweza kufadhiliwa na taasisi za fedha ili Tanzania iwe na mtiririko wa miradi yenye uwezo wa kuzalisha matokeo ya kiuchumi, kijamii na kimazingira.

