Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na aliyewahi kushika nafasi mbalimbali ndani ya Jumuiya ya Vijana, Chama pamoja na Ofisi Ndogo ya Lumumba, na kutumikia CCM katika Jiji la Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani, Mary Nchimbi, amefariki dunia Septemba 13, 2026.
Msiba huo unaendelea katika eneo la Boko Temboni, karibu na Kituo cha Watoto Yatima, Kibaha Mjini, Mkoa wa Pwani, huku taratibu za kusafirisha mwili wa marehemu kwenda mkoani Ruvuma zikiendelea.
Kwa mujibu wa taarifa za awali, mwili wa marehemu unatarajiwa kusafirishwa Jumanne, Septemba 15, 2026, kuelekea mkoani Ruvuma kwa ajili ya taratibu za maziko.
Akizungumza kuhusu marehemu, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani, Mwinshehe Mlao, alisema Nchimbi alikuwa mwanasiasa wa muda mrefu na pia mwalimu, aliyewahi kutumikia Chama Cha Mapinduzi katika Mkoa wa Pwani na kushiriki katika majukumu mbalimbali ya kiutendaji ndani ya chama.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mkoa wa Pwani, Zainab Vullu, alisema alimfahamu Nchimbi tangu miaka ya 1980, kabla ya yeye mwenyewe kuingia rasmi katika siasa, na kwamba walishirikiana katika shughuli za hamasa .
“Nimemfahamu Mary miaka ya 80 mimi nikiwa muajiriwa (Meneja uhusiano) wa shirika la uchumi la CCM SUKITA, yeye wakati huo akiwa CCM, kwenye makundi ya hamasa, kwenye mikutano wakija wajumbe wa CCM ngazi yoyote ile nilikuwa namtumia kuniletea vikundi vya hamasa (matarumbeta) “
Vullu alisema Nchimbi alikuwa kada mchapakazi wa muda mrefu, aliyejitolea na kujituma katika shughuli za chama, huku akielezwa kuwa alikuwa mtu aliyependa kuunganisha watu, asiye na majivuno wala kujiona.
Aidha, Vullu alisema Nchimbi alishiriki katika mchakato wa yeye kusimikwa kuwa mmoja wa makamanda 10 wa vijana wakati wa uongozi wa hayati Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, akiwa Mwenyekiti wa CCM Taifa.
Kwa upande wake, Katibu Mstaafu wa CCM Mkoa wa Pwani, Sauda Mpambalyoto, alisema kabla ya umauti kumfika, Nchimbi alikuwa mwanachama wa Chama cha Wastaafu wa CCM na jumuiya zake mkoani Pwani, hivyo wamepoteza mwenzao aliyekuwa mcheshi na mchapakazi.
Mpambalyoto alisema licha ya ucheshi wake, Nchimbi alikuwa mpenda watu, asiye mbaguzi na aliyekuwa akiheshimu kila mtu.
Diwani wa Viti Maalum Kibaha Mjini, Selina Wilson, alieleza Nchimbi alikuwa mtumishi na kada wa muda mrefu wa CCM, huku akimtaja kuwa dada asiye na majivuno.
Wilson alisema chama pamoja na familia wamepoteza mwanachama na mwanafamilia aliyekuwa kiungo muhimu katika masuala ya siasa na familia.
