DODOMA RS
Katika kuadhimisha na kutekeleza shughuli za Mwezi wa Maendeleo ya Jamii, Septemba 2026, Kitengo cha Maendeleo ya Jamii, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, kimewajengea uwezo wajumbe wa Kamati ya MTAKUWWA ngazi ya Mkoa, kwa lengo la kuimarisha utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto wa Miaka Mitano (2024/25–2028/29).
Mafunzo hayo yaliyobebwa na kaulimbiu “Familia Imara, Jamii Imara, Taifa Imara”, yamelenga kuwawezesha wajumbe kuelewa kwa kina maeneo ya utekelezaji wa mpango huo na kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, hususan katika kuzuia na kukabiliana na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Katika mafunzo hayo, wajumbe wamepitishwa katika maeneo nane ya utekelezaji wa MTAKUWWA ngazi ya Mkoa, yanayolenga kuimarisha uratibu wa shughuli za ulinzi na usalama wa wanawake na watoto, utoaji wa huduma kwa waathirika wa ukatili, pamoja na hatua za kuzuia ukatili katika jamii.
Aidha, mafunzo hayo yamekuwa fursa kwa wajumbe kujadili changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa mpango huo na kuweka mikakati ya pamoja ya kuhakikisha maeneo yote ya utekelezaji yanazingatiwa, ili kuongeza ufanisi katika mapambano dhidi ya ukatili.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Dodoma, Bi. Amina Mafita, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ulinzi na huduma kwa watoto walio katika mazingira hatarishi, wakiwemo watoto wa mitaani na wale wasio na makazi maalumu.
Amesema kukabiliana na changamoto hizo kunahitaji ushirikiano wa karibu baina ya Serikali, taasisi, mashirika, wadau wa maendeleo na jamii, katika kutoa elimu, kuzuia vitendo vya ukatili, kuwasaidia waathirika na kuhakikisha wahusika wanachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Wadau pia wameelekezwa kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu madhara ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto, huku wananchi wakihimizwa kutoa taarifa mara wanapobaini vitendo vya ukatili ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa wakati.
Kupitia mafunzo hayo, Kamati ya MTAKUWWA Mkoa wa Dodoma inatarajiwa kuimarisha uratibu na ushirikiano wa wadau mbalimbali katika kuzuia na kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto, pamoja na kuimarisha mifumo ya ulinzi, utoaji wa huduma na ufuatiliaji wa hatua zinazochukuliwa dhidi ya vitendo hivyo.
Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali na wadau katika kujenga familia imara, jamii salama na Taifa lenye kuheshimu haki, utu, usalama na ustawi wa wanawake na watoto.

