DODOMA RS

Mkoa wa Dodoma umekopesha jumla ya shilingi bilioni 5.9 kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupitia mikopo ya asilimia 10 katika mwaka wa fedha 2025/2026, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuwawezesha wananchi kiuchumi na kukuza shughuli za uzalishaji na ujasiriamali.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kitengo cha Maendeleo ya Jamii, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Bi. Rennie Gondwe, wakati akifunga mafunzo ya siku nne kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii na Maafisa Biashara kutoka Halmashauri za Mkoa wa Dodoma yaliyolenga kuwaongezea ujuzi kuhusu utoaji na urejeshaji wa mikopo ya asilimia 10. Mafunzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Kampasi ya Dodoma, Septemba 11, 2026.

Bi. Gondwe amesema kati ya shilingi bilioni 5.9 zilizokopeshwa, vikundi vya wanawake vilipokea shilingi bilioni 2.8, vijana shilingi bilioni 2.9, huku vikundi vya watu wenye ulemavu vikipokea shilingi milioni 172.67.

“Takwimu hizi zinaonesha ukubwa wa dhamana tuliyopewa ya kuhakikisha mikopo inawafikia walengwa, inatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na inarejeshwa kwa wakati ili kuwawezesha wengine pia kunufaika,” amesema Bi. Gondwe.

Amesema utekelezaji wa mikopo hiyo unaendana na azma ya Serikali ya kujenga uchumi jumuishi na wenye ushindani kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, huku Maafisa Maendeleo ya Jamii wakiwa miongoni mwa chachu muhimu katika kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Amewataka Maafisa Maendeleo ya Jamii na Maafisa Biashara kuhakikisha utoaji wa mikopo unafanyika kwa uwazi na kwa kuzingatia taratibu, sambamba na kuimarisha ufuatiliaji wa matumizi ya fedha ili miradi inayotekelezwa na vikundi iwe na tija, iwe endelevu na iweze kuongeza kipato kwa wanufaika.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa CBE Kampasi ya Dodoma, Dkt. Josephine Chuck, amesema Chuo hicho kimeendesha mafunzo hayo kwa kutekeleza maelekezo ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, baada ya kubaini matokeo chanya ya mafunzo yaliyotolewa awali.

Amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo Maafisa Maendeleo ya Jamii na Maafisa Biashara ili waweze kuboresha zaidi usimamizi na utoaji wa mikopo ya asilimia 10 na kuhakikisha inawanufaisha walengwa kwa ufanisi.

Aidha, Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Bi. Monica Chisongela, amesema mikopo hiyo ni chachu muhimu ya kuinua uchumi wa wananchi, hivyo mafunzo hayo yatawawezesha Maafisa kupata mbinu bora za kuwasaidia wanufaika kuendesha na kuboresha miradi yao kwa tija na uendelevu.

Mafunzo hayo yamehitimishwa kwa maazimio mbalimbali, yakiwemo kuwawezesha Maafisa Maendeleo ya Jamii ambao hawakupata nafasi ya kushiriki mafunzo hayo kupata mafunzo katika awamu nyingine, kuendelea kutoa elimu kwa vikundi vinavyotarajia kuomba mikopo pamoja na vile ambavyo tayari vimepata mikopo.

Maazimio mengine ni kuimarisha ufuatiliaji wa vikundi mara baada ya kupokea mikopo ili kubaini mapema changamoto zinazoweza kujitokeza na kuhakikisha vikundi vinaendelea kupewa ushauri na malezi kabla na baada ya kupata mikopo.

Hatua hizo zinalenga kuhakikisha mikopo ya asilimia 10 inaendelea kuwa nyenzo madhubuti ya uwezeshaji wa wananchi, ukuaji wa biashara na ujenzi wa uchumi jumuishi na endelevu katika Mkoa wa Dodoma.