Na Sophia Kingimali, Dar es Salaam

SERIKALI imetangaza nafasi 150 za wanafunzi wa Kitanzania waliofanya vizuri katika masomo ya sayansi kupata ufadhili wa masomo nchini Algeria, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuwawezesha vijana wenye uwezo kupata elimu nje ya nchi na kujenga wataalamu watakaosaidia maendeleo ya Taifa.

Akizungumza kuhusu fursa hiyo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Adolf Mkenda amesema wanafunzi hao watachaguliwa miongoni mwa waliokuwa wamepata Samia Scholarship ya STEM ya kusoma katika vyuo vya ndani, huku kigezo kikuu kikiwa ni ufaulu wao katika masomo ya sayansi bila kujali uwezo wa kifedha wa familia zao.

Amesema, wanafunzi hao 150 waliofanya vizuri zaidi watawasiliana nao kuanzia sasa na kupewa nafasi ya kuamua kama wako tayari kwenda Algeria kwa ajili ya masomo ya elimu ya juu katika vyuo vya Serikali ya nchi hiyo.

Ameeleza kuwa Serikali ya Algeria itagharamia ada za masomo ya wanafunzi hao, huku Serikali ya Tanzania kupitia mpango wa Samia Scholarship ikigharamia mahitaji ya maisha yao kwa kuongeza fedha zitakazowawezesha kuishi nchini humo wakati wa masomo.

Hatua hiyo inalenga kuondoa changamoto ambayo imekuwa ikiwakabili wanafunzi wenye ufaulu mzuri lakini wanashindwa kwenda kusoma nje ya nchi kutokana na kushindwa kumudu gharama za maisha, licha ya kupata nafasi za masomo zinazolipiwa ada.

Ameongeza kuwa wanafunzi hao watatakiwa kujiandaa pia kujifunza lugha ya Kifaransa kwa kuwa sehemu kubwa ya masomo nchini Algeria hutolewa kwa lugha hiyo, huku wakipata fursa ya kuongeza ujuzi wa lugha ya kimataifa pamoja na elimu katika nyanja mbalimbali za sayansi na teknolojia.

Wanafunzi hao wanatoka katika orodha ya wanafunzi 1,000 waliotangazwa awali kupata Samia Scholarship ya STEM kwa ajili ya kusoma katika vyuo vya ndani, ambapo 10 tayari wamechaguliwa kwenda Moscow, Urusi, baada ya Tanzania kupata nafasi za masomo kutoka nchi hiyo.

Serikali imeeleza kuwa baada ya wanafunzi 10 kwenda Urusi, wanafunzi 990 watabaki katika mpango wa masomo ya ndani, lakini baadhi yao wataendelea kuchaguliwa kupata fursa nyingine za masomo nje ya nchi kulingana na ufaulu wao.

Aidha, Serikali imesema kuna uwezekano wa wanafunzi wengine 15 kutoka kundi hilo kupata fursa za kusoma nje ya nchi, huku taarifa zaidi kuhusu nafasi hizo ikitarajiwa kutolewa baada ya taratibu za maandalizi kukamilika.

Aidha Prof.Mkenda amesema kuwa uteuzi wa wanafunzi unafanywa kwa kuzingatia ufaulu na vigezo vinavyoweza kuthibitishwa, ili kuhakikisha fedha za Serikali zinatumika kuwawezesha wanafunzi wenye uwezo mkubwa kitaaluma bila upendeleo.

Serikali pia imesisitiza kuwa inalenga kutumia fursa za masomo nje ya nchi kujenga wataalamu katika maeneo yenye mahitaji makubwa, yakiwemo sayansi ya data, akili bandia (Artificial Intelligence), machine learning, teknolojia ya habari, uhandisi na tiba.

Sambamba na hayo,Amesema Serikali inaendelea kufanya mazungumzo na nchi nyingine zinazotoa nafasi za masomo kwa Watanzania ili kuhakikisha fursa hizo zinatangazwa kwa umma na wanafunzi wanaostahili wanapata nafasi bila kujali hali zao za kiuchumi.

Hatua hiyo inaelezwa kuwa ni sehemu ya utekelezaji wa msukumo wa Serikali wa kuwapeleka Watanzania kusoma katika nchi mbalimbali duniani, kupata elimu na uzoefu wa kimataifa, kisha kutumia ujuzi huo katika kuchangia maendeleo ya Tanzania.