NA DENIS MLOWE, IRINGA

MKURUGENZI wa Bodi ya Maji Bonde la Rufiji, David Munkyala, amesema Serikali imeanza kuchukua hatua za kudumu katika kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa maji kwa mifugo na migogoro kati ya wakulima na wafugaji katika Tarafa ya Pawaga, Wilaya ya Iringa.

Munkyala amesema hayo wakati akizungumza na wanahabari juu ya hatua zilizochukuliwa na Bodi hiyo katika kuhakikisha wafugaji wanapata maji kwa ajili ya mifugo yao bila kulazimika kuingia katika maeneo ya mashamba au kutumia vyanzo vya maji vilivyopo kwenye maeneo ya miradi ya umwagiliaji.

Amesema changamoto hiyo ilijitokeza zaidi baada ya kuboreshwa kwa Skimu ya Umwagiliaji ya Mkombozi, ambapo awali wafugaji walikuwa wakipeleka mifugo kunywa maji katika maeneo ya mto na mabondeni, lakini baada ya maboresho ya skimu hiyo utaratibu huo ukabadilika na wafugaji kuzuiwa kupeleka mifugo katika maeneo ya mradi.

Munkyala alisema kuwa hali hiyo ilisababisha baadhi ya wafugaji kukosa maeneo mbadala ya kunyweshea mifugo na hivyo kuanza kuingia katika maeneo ya mashamba ya wakulima, jambo lililokuwa likichochea migogoro kati ya makundi hayo.

Amesema baada ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, kutoa maelekezo mwezi Julai mwaka huu ya kutafutwa kwa njia mbadala ya kuwapatia wafugaji maji, Bodi ya Maji Bonde la Rufiji ilifanya utafiti na kuanza utekelezaji wa hatua hiyo kwa kuchimba kisima kirefu katika eneo hilo.

“Tumefanya survey na kuchimba kisima kirefu cha zaidi ya mita 100 na tumefanikiwa kupata maji ya kutosha. Kisima hiki kinatoa takribani lita 15 kwa sekunde, ambayo ni kiwango kikubwa cha maji,” amesema Munkyala.

Ameeleza kuwa lengo la kuchimba kisima hicho lilikuwa ni kuhakikisha wafugaji wanapata maji karibu na maeneo yao, hatua ambayo itasaidia kupunguza migogoro kati yao na wakulima, sambamba na kulinda vyanzo vya maji na mazingira.

Munkyala amesema matumizi ya mito na mabonde kwa ajili ya kunyweshea mifugo yanaweza kusababisha uharibifu wa kingo za mito, mmomonyoko wa udongo na kuongezeka kwa tope kwenye mito, hali ambayo inaweza kupunguza kina cha maji na kuathiri matumizi ya maji kwa shughuli mbalimbali, ikiwemo umwagiliaji na uzalishaji wa nishati.

“Kitendo cha mifugo kwenda mtoni kinaweza kuharibu kingo za mto na kusababisha mmomonyoko wa udongo na udongo huo huingia mtoni na kuongeza matope, jambo ambalo linaweza kupunguza kina cha mto na kuathiri matumizi ya maji kwa shughuli nyingine,” amesema.

Amesema ujio wa Mawaziri wawili wenye dhamana ya sekta ya kilimo pamoja na mifugo na uvuvi katika eneo hilo ni hatua muhimu kwa kuwa wamekuja kujionea utekelezaji wa mradi huo na kutafuta suluhisho la kudumu la changamoto zinazowakabili wakulima na wafugaji.

Munkyala, hatua zilizopendekezwa na Mawaziri hao zimeongeza matumaini ya kumaliza changamoto hiyo, baada ya kuahidi kuongeza miundombinu katika kisima kilichochimbwa pamoja na kuchimba visima vingine vitano kwa ajili ya kuwapatia wananchi na wafugaji maji.

Amesema kati ya visima hivyo, vitatu vinatarajiwa kuanza kuchimbwa kwa haraka na kuwezeshwa kwa miundombinu inayohitajika ili viweze kutumika na wananchi pamoja na wafugaji.

Amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza utegemezi wa mifugo kwenda kwenye mabonde na mito kutafuta maji, hali ambayo imekuwa ikichangia migogoro na uharibifu wa mazingira.

Aidha, amesema Mawaziri hao wameelekeza Halmashauri kuhakikisha zinajenga miundombinu maalumu ya kunyweshea mifugo, huku zikitafutwa pia njia za kuongeza upatikanaji wa malisho kwa wafugaji.

Amesema miongoni mwa mikakati hiyo ni kuwezesha upandaji wa nyasi na kuboresha maeneo ya malisho ili mifugo ipate chakula cha kutosha na kupunguza ulazima wa wafugaji kupeleka mifugo katika maeneo ya mabondeni kwa ajili ya kutafuta maji na malisho.

Munkyala amewashukuru Mawaziri hao kwa kutembelea eneo la mradi na kutoa maelekezo yanayolenga kupata suluhisho la kudumu, akisema hatua hizo zitasaidia kuimarisha mahusiano kati ya wakulima na wafugaji, kulinda mazingira na kuhakikisha rasilimali za maji zinatumika kwa uendelevu.