Na Mwandishi Wetu WMJJWM- Dodoma

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii na Makundi Maalum, 

Wakili Amon Mpanju, amewataka wadau wa maendeleo hususani wanaojishughulisha na watoto, kugawana maeneo ya kufanyia kazi badala ya kujikita eneo moja.

Mpanju ameyasema hayo wakati akizindua kanuni za uanzishaji, uendeshaji na uratibu wa Mabaraza ya Watoto nchini, Septemba 11, 2026 jijini Dodoma.

Akieleza zaidi kuhusu kauli hiyo, Mpanju amesema, matarajio ya Serikali ni kuzindua Mabaraza ya watoto nchi nzima, hivyo ni vema wadau kupeana maeneo tofauti ili kurahisisha uratibu wa mabaraza hayo kwenye kila eneo.

“Isiwe ni maneno ya Jukwaani tu, tufanye “mapping” (ramani) ili kujua nani anafanya nini na wapi kuhakikisha utekelezaji wa mabaraza unafanyika kwa ufanisi, kuanzia uanzishwaji, uendeshaji, ufuatiliaji na Tathmini. Lengo la mabaraza ni kuendeleza watoto wetu, kujua haki zao, kutambua vipaji vyao na kuwaandaalia kesho yao” amesema Wakili Mpanju.

Aidha, amewaelekeza watendaji kuanzia ngazi ya Wizara kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kuhakikisha Mabaraza ya Watoto yanaanzishwa na wadau wanakuwa na ramani ya namna ya kuratibu utendaji kazi wa mabaraza hayo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Watoto Daniel Magembe, ameishukuru Serikali kwa kuhakikisha mabaraza ya watoto yanatambulika kisheria na ameomba kuzingatiwa kwa utengaji wa bajeti katika utekelezaji wa majukumu ya mabaraza hayo.

Magembe amesema mapendekezo mbalimbali yaliyojadiliwa na Kamati Kuu ya Baraza la Watoto, ikiwemo kuboreshwa kwa sheria ya ndoa ya mwaka 1971 hasa eneo la umri wa kuolewa na maboresho ya miundombinu inayoendana na wakati wa sasa.