Na Sophia Kingimali, Dar es Salaam

WATANZANIA wamehamasishwa kujitokeza kwa wingi kushiriki programu ya “Twenzetu Kileleni” kwa kupanda Mlima Kilimanjaro pamoja na kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha utalii wa ndani na uhifadhi wa mazingira.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba10,2026 wakati akizindua kampeni ya TWENDEZETU KILELENI msimu wa tano, Mkurugenzi wa Zara Tanzania Adventures, Zainab Ansell, amesema msimu wa tano unatarajiwa kuwakutanisha zaidi ya watu 200 watakaopanda Mlima Kilimanjaro, huku vijana watakaowaunga mkono wakifanya idadi ya washiriki kuwa zaidi ya watu 400.

Amesema programu hiyo inalenga kuwafanya Watanzania kutambua thamani ya vivutio vya utalii vilivyopo nchini, akibainisha kuwa wageni kutoka nje ya nchi wamekuwa wakifika kwa wingi kupanda Kilimanjaro, hivyo ni wakati kwa Watanzania wenyewe kutumia fursa hiyo kujivunia rasilimali zao.

Ansell amesema kabla ya kupanda mlima huo, washiriki watashirikishwa katika programu ya uhifadhi wa mazingira, ikiwamo upandaji miti, kwa lengo la kuhakikisha Kilimanjaro inaendelea kuwa rasilimali salama kwa vizazi vijavyo.

Alisema Watanzania ambao hawataweza kushiriki zoezi la kupanda mlima wataweza kuungana na wenzao katika safari ya Serengeti, Lake Manyara, Ngorongoro na maeneo mengine ya utalii, hatua ambayo itawapa fursa ya kujionea vivutio hivyo kwa gharama nafuu.

Mkurugenzi huyo amesema kampuni hiyo itaendelea kushirikiana na jamii kupitia miradi mbalimbali, ikiwamo kusaidia elimu na upandaji miti, huku akiwataka Watanzania kutumia mwezi Desemba kutembelea Kilimanjaro na Serengeti ili kujionea utajiri wa utalii uliopo nchini.

Kwa upande wake, Faustin John kutoka Zara Tanzania Adventures, alisema kampuni hiyo imejiandaa kuhakikisha wapandaji wanapata huduma bora, zikiwamo mavazi, malazi, chakula, waongozaji wenye ujuzi na elimu kuhusu rasilimali zinazopatikana ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro.

Amesema wamechagua njia ya Marangu kwa kuwa ina miundombinu ya malazi na inafaa kwa kipindi cha mvua kinachotarajiwa, huku washiriki wakipanga kutumia siku sita katika safari hiyo ili kupata nafasi ya kufurahia mazingira na kufikia kilele.

Aidha John, ametoa wahamasisha viongozi wa serikali, wabunge, mawaziri, taasisi binafsi, taasisi za dini, mabalozi na Watanzania kwa ujumla kujitokeza na kushiriki programu hiyo ili kuonyesha mfano wa matumizi ya vivutio vya utalii vya ndani.

Aidha, alisema Zara Tanzania Adventures ina uzoefu wa miaka 40 katika kuendesha shughuli za utalii na imejipanga kutoa huduma pia kwa watu wenye mahitaji maalumu wanaotaka kushiriki safari za utalii.

Naye Peter Mwambuga kutoka TTCL amesema huduma za mawasiliano zimeboreshwa katika eneo la Mlima Kilimanjaro, ikiwamo uwezo wa mawasiliano kuanzia geti la Marangu hadi kileleni, jambo litakalosaidia washiriki kupata huduma za mawasiliano wakati wa safari.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Chuo cha Taifa cha Utalii Mary Maduhu alisema programu hiyo ni fursa kwa wanafunzi na wafanyakazi kupata uzoefu wa moja kwa moja katika utalii wa milimani, uhifadhi na usimamizi wa urithi wa Taifa.