Meneja wa kampuni hiyo Afrika , Andrea Giacalone akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha kuhusiana na teknolojia hiyo ya “Baby Checker”.

Mwakilishi kutoka kampuni hiyo nchini Tanzania, Dkt. Deogratius Mzurikwao, akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha

…….

Na Happy Lazaro, Arusha 

Kampuni ya DELFT IMAGING inayojihusisha na maswala ya utaalamu wa Afya kutoka Netherlands imekuja na teknolojia ya kisasa inayotumia akili bandia (AI) katika uchunguzi wa afya ya mama mjamzito na mtoto, kupitia kifaa cha ultrasound kinachojulikana kama “Baby Checker”, kinacholenga kuongeza upatikanaji wa huduma za uchunguzi, hususani katika maeneo yenye upungufu wa wataalamu na vifaa tiba.

Akizungumza kuhusu teknolojia hiyo, Meneja wa kampuni hiyo Afrika , Andrea Giacalone Andrea amesema teknolojia hiyo ya “Baby Checker “ni kifaa rahisi kutumia kinachounganishwa na simu ya mkononi kupitia probe maalumu na haitumii huduma ya internet na kumwezesha mhudumu wa afya kufanya uchunguzi wa awali wa mama mjamzito hata katika maeneo ambayo hayana huduma za ultrasound.

Amesema kuwa,kifaa hicho kinaweza kutoa taarifa muhimu kuhusu ujauzito, ikiwemo umri wa ujauzito, mkao wa mtoto tumboni, mahali lilipo kondo la nyuma (placenta) pamoja na idadi ya watoto waliopo tumboni, hivyo kusaidia wahudumu wa afya kufanya tathmini ya awali kwa wakati.

Andrea amesema teknolojia hiyo inalenga zaidi kusaidia jamii za vijijini na maeneo ya mbali ambako upatikanaji wa huduma za ultrasound na wataalamu wa afya ni changamoto, akisisitiza umuhimu wa kuwawezesha wahudumu wa afya kutumia teknolojia rahisi na zinazoweza kufikishwa katika maeneo yenye uhitaji.

“Delft Imaging pia inashirikiana na Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu, ambapo Tanzania imeanza kutumia mashine 10 za X-ray zinazobebeka zenye programu ya AI inayosaidia katika uchunguzi wa kifua kikuu, hususan kupitia shughuli za active case finding.”amesema Andrea .

Ameeleza kuwa vifaa hivyo vinasaidia kuwafikia wananchi katika jamii na kubaini wagonjwa wa kifua kikuu ambao huenda wasifike katika vituo vya afya, huku teknolojia hiyo ikiwa sehemu ya juhudi za kuongeza ufanisi wa uchunguzi katika maeneo yenye changamoto ya upatikanaji wa huduma.

“Safari ya Delft Imaging barani Afrika ilianza mwaka 1996 kupitia ushirikiano kati ya Radboud University ya Uholanzi na Lung Institute of Cape Town, ambapo kampuni hiyo ilianza kutengeneza programu za computer-aided detection zilizolenga kuwasaidia wahudumu wa afya katika uchunguzi wa kifua kikuu.”amesema .

Amesema kupitia ushirikiano na Global Fund pamoja na washirika wengine wa kimataifa, Delft Imaging imeweza kufanya kazi katika zaidi ya nchi 90 duniani, huku teknolojia ya Baby Checker ikiwa tayari imetekelezwa katika nchi zaidi ya 17 barani Afrika.

Kwa upande wake, Mwakilishi kutoka kampuni hiyo nchini Tanzania, Dkt. Deogratius Mzurikwao, amesema kampuni hiyo imekuwa ikifanya kazi nchini kwa takribani miaka mitano na tayari ina bidhaa zaidi ya nne zinazolenga kurahisisha huduma za uchunguzi wa magonjwa mbalimbali.

Dkt. Mzurikwao amesema miongoni mwa teknolojia hizo ni Delft Light, kifaa cha X-ray kinachobebeka ambacho kinaweza kusafirishwa hadi maeneo ya mbali, hata kwa kutumia bodaboda, na kufanya uchunguzi wa kifua kikuu bila kuhitaji intaneti, huku bidhaa hiyo ikiwa tayari inatumika katika maeneo 32 nchini kwa kushirikiana na Wizara ya Afya.

Amesema teknolojia ya “Baby Checker” imeundwa kwa kuzingatia changamoto zinazowakabili wanawake wajawazito, ambapo mtumiaji hupatiwa maelekezo ya video ya takribani dakika tatu na anaweza kufanya uchunguzi ndani ya takribani dakika mbili kwa kutumia simu ya mkononi pamoja na kifaa hicho.

“Ukiangalia kuna vifo vingi vinatokea kwa mama mjamzito kwa sababu hapati uwezo wa kufika hospitali kwa wakati na wakati mwingine huduma ya ultrasound haipatikani kwa urahisi hivyo teknolojia hii ni portable, unachohitaji ni simu ya mkononi na kifaa hiki,” amesema Dkt. Mzurikwao.

Amesema kifaa hicho cha ultrasound kinauzwa kwa takribani dola 5,000, ambapo kinawafikia wateja wanaohitaji mahali popote pale walipo kwa urahisi na wakati pamoja na kutoa mafunzo ya matumizi na msaada wa kitaalamu.

Dkt Mzurikwao amesema kampuni hiyo inalenga kuanza majadiliano na TAMISEMI na Wizara ya Afya ili kujenga ushahidi wa matumizi ya teknolojia hiyo nchini na kupata mrejesho wa mamlaka kabla ya kuitekeleza kwa kiwango kikubwa.