Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
Septemba 9, 2026
WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema Mkoa wa Pwani umewekwa kuwa kituo kikuu cha kuhifadhi vifaa vya dharura vitakavyotumika kukabiliana na athari za mvua za El Nino.
Amebainisha vituo vingine vimewekwa katika Kanda ya Kati-Dodoma, Kanda ya Ziwa na Nyanda za Juu Kusini, huku Pwani ikiwa kituo kikuu cha kuhifadhi vifaa hivyo.
Ulega ameeleza hayo alipowasili mkoani Pwani kwa ajili ya kutekeleza maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kujiandaa mapema kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua hizo.
Amesema vifaa vilivyohifadhiwa Pwani, vikiwemo makaravati ya chuma, vikapu vya mawe na madaraja ya chuma, vinapaswa kuwa tayari kutumika wakati wowote, huku akisisitiza ukaguzi na usafishaji wa mitaro, makaravati na madaraja ili kuhakikisha maji yanapita kwa uhuru na kuzuia barabara kukatika.
Ulega ameiagiza Wakala wa Barabara Tanzania, TANROADS, na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini, TARURA, kuhakikisha wanakagua madaraja na mitaro yote nchini, kuzibua mitaro pamoja na makaravati ili kuruhusu maji kupita kwa urahisi.
Aidha, amezitaka TANROADS na TARURA kufanya tathmini za mara kwa mara katika maeneo hatarishi, akisisitiza tathmini hizo kufanyika kila wiki ili kuongeza nguvu katika maeneo ambayo yanaweza kuzidiwa na mvua na kuhakikisha hakuna barabara inayofungwa.
Katika hatua nyingine, amemtaka Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani kusimamia wakandarasi ambao hawajalipwa, huku akiwataka wakandarasi kuendelea na utekelezaji wa majukumu yao na kutoa ushirikiano katika kipindi hiki cha maandalizi.
Meneja wa TANROADS Pwani, Mhandisi Joel Mwambungu, amesema wamejipanga katika mikoa yote 26 inayosimamiwa na TANROADS, ikiwemo kusafisha madaraja, mitaro na makaravati.
Ameeleza eneo la Ruvu Chini na Daraja la Mto Mpiji ni miongoni mwa maeneo yanayofanyiwa kazi, ambapo wanaendelea kusafisha kingo za mto ili kuruhusu maji kupita kwa kiwango kilichosanifiwa.
Mwambungu amesema vifaa vilivyopo ni pamoja na makaravati ya chuma yenye urefu wa mita 5,638, sawa na makaravati 568, pamoja na vikapu vipande 4,240, ambavyo vitatumika endapo barabara au madaraja yatapata hitilafu.
Amesema pia kuna madaraja makubwa saba, karavati za plastiki zenye urefu wa mita 1,200, sawa na karavati 120, pamoja na karavati za chuma zenye urefu wa mita 1,500, sawa na karavati 150.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Shaibu Ndemanga, ametoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari katika maeneo wanayoishi, akiwataka wanaoishi mabondeni kuondoka ili kujikinga na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua hizo.

