Serikali imekipongeza Chama cha Wanawake Wahasibu Tanzania (TAWCA), kwa mchango wake katika tasnia ya uhasibu nchini lakini pia kwa kuimarika na kuwa taasisi muhimu katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi nchini.
Pongezi hizo zimetolewa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), wakati akifungua Mkutano wa Tisa wa Chama cha Wanawake Wahasibu -TAWCA wenye kaulimbiu “Uongozi unaozingatia kuacha alama katika enzi ya kidijitali: Ubunifu wenye uadilifu kwa matokeo endelevu”, kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), katika hoteli ya Malaika Resort, jijini Mwanza.
Mhe. Munde alisema kuwa, maendeleo ya chama hicho kutoka kundi la waanzilishi 18 hadi kuwa na zaidi ya wanachama hai 1,200 ni ishara ya uwezo wa wanawake wataalamu katika kujenga taasisi imara na kuchangia maendeleo ya taifa.
Alisema TAWCA imevuka mipaka ya kuwa chama cha kitaaluma pekee na sasa imekuwa sehemu muhimu ya juhudi za kujenga uwezo wa kiuchumi, kukuza rasilimali watu na kuimarisha usimamizi wa fedha nchini.
“Jitihada mbalimbali zinazofanywa na TAWCA katika kuwawezesha wanawake kiuchumi, ni dhahiri kuwa unaendana na juhudi za Serikali za kuimarisha matumizi ya teknolojia katika usimamizi wa fedha za umma, kuongeza uwazi na kudhibiti upotevu wa rasilimali, na zinaunga mkono azma ya Serikali kufikia ujumuishaji wa kiuchumi unaowanufaisha wananchi kuanzia ngazi ya chini” aliseme Mhe. Munde
Mhe. Munde alisema kuwa kupitia mpango wa “Bado Naweza”, wa TAWCA imewajengea uwezo wa kibiashara wanawake vijana 101, kutoa mwongozo kwa wafanyabiashara wanawake 208, kufanikisha kiwango cha urejeshaji wa mikopo kufikia asilimia 96, kuongeza mfuko wa TAWCA SACCOS hadi zaidi ya Shilingi milioni 520, hatua ambayo inasaidia kujenga uwezo wa wanachama na kuongeza mtaji wa ndani.
“Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Serikali kwa ujumla, ninaahidi kuendelea kuiunga mkono TAWCA na kutoa wito kwa Wizara, taasisi za Serikali, washirika wa maendeleo, wafanyabiashara na wadhamini kushirikiana na chama hicho katika kutekeleza programu zake” alisema Mhe. Munde
Mhe. Munde aliwataka washiriki wa mkutano huo kutumia jukwaa hilo kujadili mawazo mapya na ya kijasiri katika masuala ya fedha, kuimarisha ushauri kati ya vizazi na kuweka hatua madhubuti za kuendeleza taaluma ya uhasibu kwa kuzingatia viwango vya juu vya uadilifu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wahasibu (TAWCA), CPA Mary Mabiti, alieleza kuwa safari ya chama hicho imejengwa katika misingi ya ushirikiano, uwezeshaji na kujenga uwezo wa wanawake katika taaluma ya uhasibu.
Alisema tangu kuanzishwa kwake mwaka 2015, TAWCA imeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuwaunganisha wanawake wataalamu wa uhasibu, kuwawezesha vijana kupitia mafunzo, programu za mafunzo kwa vitendo na maendeleo ya taaluma, huku ikisisitiza umuhimu wa kujifunza kwa kuendelea, ubunifu na kuendana na mabadiliko ya mazingira ya biashara ya kimataifa.
“Mafanikio yaliyofikiwa yamechangiwa na ushirikiano kati ya TAWCA, Serikali, Bodi ya Uhasibu Tanzania -NBAA, taasisi mbalimbali, washirika na wadau, nguvu ya pamoja ni muhimu katika kuendeleza taaluma, kuwawezesha wanawake na kuchangia maendeleo ya Taifa” alisema Bi. Mabiti
Naye Mlezi wa TAWCA ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), CPA Prof. Siasa Mzenzi, amekihakikishia Chama hicho ushirikiano na msaada wa Serikali katika kuendeleza na kutekeleza mipango yake ya kukuza taaluma ya uhasibu nchini.
CPA. Prof. Mzenzi aliitaka TAWCA kujifunza kutoka kwa taasisi na jumuiya za kitaaluma zinazofanya vizuri barani Afrika, huku Tanzania ikitumia fursa hiyo kubadilishana uzoefu na mbinu bora katika kuimarisha taasisi hiyo na kujenga jumuiya ya wataalamu wa uhasibu iliyo imara, jumuishi na yenye mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa.

