Na Sophia Kingimali, Dar es Salaam
CHUO cha Bahari Dar es Salaam (DMI) kimesisitiza umuhimu wa kuunganisha elimu, utafiti, teknolojia na mahitaji ya sekta ili kuhakikisha fursa zinazopatikana katika uchumi wa buluu zinageuka kuwa ajira, uwekezaji na manufaa kwa wananchi.
Mwenyekiti wa Bodi ya DMI, Peter Olekashe, alisema hayo leo Septemba 9, 2026, wakati akifunga Kongamano la Tano la Kimataifa la Uchumi wa Buluu lililofanyika jijini Dar es Salaam, akieleza kuwa ushirikiano kati ya taasisi za elimu na viwanda ni muhimu katika kutatua changamoto zinazoikabili sekta hiyo.
Amesema tafiti zinazofanywa na vyuo vikuu na taasisi za utafiti zinapaswa kuhusishwa moja kwa moja na changamoto zilizopo katika sekta ya uchumi wa buluu ili matokeo yake yaweze kutumika katika kuboresha uzalishaji na kuongeza manufaa ya kiuchumi.
Olekashe amesema wadau wa sekta wanapaswa kuwasilisha changamoto zao kwa taasisi za kisayansi ili watafiti wapate maeneo ya kufanyia tafiti na kubuni suluhisho badala ya tafiti hizo kubaki kwenye vitabu na maktaba bila kutumika.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kusambaza matokeo na maazimio ya kongamano hilo kwa wananchi wengi zaidi, akisema DMI inapaswa kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano (ICT) kuhakikisha taarifa hizo zinawafikia hata wananchi ambao hawakupata nafasi ya kushiriki kongamano.
Kwa upande wake, Mkuu wa chuo cha DMI, Prof. Tumaini Gurumo, amesema kongamano hilo lililofanyika kwa siku tatu kuanzia Septemba 7 hadi 9, lilijadili maeneo mbalimbali yanayohusu maendeleo ya uchumi wa buluu, ikiwemo elimu, uhifadhi wa rasilimali, uwekezaji na ujasiriamali.
Amesema mjadala wa siku ya kwanza ulijikita katika elimu, mafunzo na ujenzi wa rasilimali watu yenye ujuzi unaohitajika katika uchumi wa buluu, sambamba na umuhimu wa kutunza rasilimali za baharini na maji ili ziendelee kuwa na manufaa kwa vizazi vijavyo.
Prof. Gurumo amesema siku ya pili ilijikita katika uwekezaji na ujasiriamali, ambapo ilibainika kuwa wajasiriamali wengi katika sekta ya uchumi wa buluu wanahitaji uwezeshwaji wa kifedha ili kukuza shughuli zao.
Sambamba na hayo amezitaka taasisi za fedha kubuni mifumo rafiki ya kuwawezesha wajasiriamali hao, ikiwemo mikopo inayozingatia mahitaji na mazingira ya shughuli zinazofanyika katika uchumi wa buluu.
Katika eneo la teknolojia, Prof. Gurumo amesema kuna umuhimu wa taasisi za elimu na mafunzo ya bahari kuwekeza katika teknolojia za kisasa ili wahitimu wawe na uwezo wa kukabiliana na mahitaji ya soko la ajira la ndani na kimataifa.
Amesema matumizi ya teknolojia zilizopitwa na wakati katika mafunzo yanaweza kuwafanya wahitimu kukumbana na changamoto wanapoingia katika maeneo ya kazi yanayotumia mifumo ya kisasa, hali inayoweza kuongeza hatari za ajali na uharibifu.
Akizungumzia siku ya tatu ya kongamano hilo, Prof. Gurumo alisema washiriki walijadili masuala ya sheria na sera zinazohusiana na uchumi wa buluu, ikiwemo utekelezaji wa mikataba ya kimataifa kuhusu bahari, huku akisisitiza kuwa mipango bila utekelezaji haiwezi kuleta matokeo yaliyokusudiwa.
Amesema moja ya maazimio muhimu ya kongamano hilo ni kuongeza elimu kwa wananchi kuhusu uchumi wa buluu kuanzia ngazi za jamii hadi Taifa, pamoja na kuimarisha mafunzo rasmi yatakayozalisha wataalamu wenye ujuzi unaoendana na mahitaji ya sekta.

