Na Sophia Kingimali, Dar es Salaam

WIZARA ya Katiba na Sheria imesisitiza umuhimu wa kuoanisha sheria za Tanzania na sheria za kimataifa ili kuimarisha usimamizi wa rasilimali za bahari na kuhakikisha uchumi wa bluu unakuwa endelevu kwa manufaa ya Taifa.

Akizungumza wakati wa Kongamano la Tano la Kimataifa la Uchumi wa Bluu lililofanyika jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa kitengo cha utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala Wizara ya Katiba na Sheria, Felix Chakila, amesema wizara hiyo ilishiriki kongamano hilo kwa kuzingatia wajibu wake wa kikatiba wa kulinda na kusimamia maliasili za nchi.

Amesema kongamano hilo lililofanyika kwa siku tatu kuanzia Septemba 7 hadi 9, 2026, limekuwa fursa kwa Tanzania kupata mawazo na maoni kutoka kwa wadau mbalimbali kuhusu namna bora ya kuimarisha sekta ya maliasili na kuweka mazingira ya kisheria yatakayowezesha utekelezaji wa Uchumi wa Bluu kwa kuzingatia Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.

Chakila alisema moja ya mambo yaliyoibuliwa katika kongamano hilo ni umuhimu wa kuhakikisha sheria za ndani zinaendana na sheria za kimataifa, hatua ambayo itasaidia kuzuia migongano ya kisheria katika mahusiano ya kimataifa, ikiwemo masuala yanayohusu nchi na nchi pamoja na mahusiano ya watu binafsi.

Kwa mujibu wa Chakila, Tanzania ina sheria mbalimbali zinazohusiana na ulinzi na usimamizi wa maliasili, mipaka na rasilimali za bahari, hivyo kuna umuhimu wa kuendelea kuzihuisha na kuhakikisha zinakidhi mahitaji ya sasa ya uchumi wa bluu.

Kwa upande wake, Kamishna anayesimamia Kitengo cha Katiba na Sheria wa Taasisi ya Wanafunzi wa Vyuo na vyuo vikuu Tanzania (TAHLISO) Aron Seni alisema ushiriki wao katika kongamano hilo umewawezesha kujifunza namna Wizara ya Katiba na Sheria inavyotekeleza majukumu yake katika kusimamia Katiba na sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikiwemo sheria zinazosimamia masuala ya bahari.

Amesema wamejifunza pia kuhusu huduma ya msaada wa kisheria inayotolewa kupitia mpango wa Msaada wa Kisheria wa Mama Samia, ambao umewawezesha wananchi wenye changamoto za kifedha kupata huduma za kisheria na kusaidiwa kutatua migogoro yao.

Aidha, amesema masuala ya bahari yanaongozwa kwa kiasi kikubwa na sheria za kimataifa, huku akisisitiza umuhimu wa Tanzania kuendelea kufanya domestication ya sheria hizo kwa kuzifanyia utekelezaji kupitia sheria za ndani ili kuongeza nguvu katika usimamizi na ulinzi wa rasilimali za bahari.

Amesema hatua hiyo ni muhimu kutokana na nafasi kubwa ya uchumi wa bluu katika kukuza shughuli za usafirishaji, uvuvi, upatikanaji wa chakula, utalii na shughuli nyingine za kiuchumi zinazotegemea bahari, hivyo sheria imara na utekelezaji wake ni msingi wa kuhakikisha rasilimali hizo zinatumika kwa njia endelevu.