Na John Walter -Babati
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Manyara kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi limewakamata watu watatu kutoka Kitongoji cha Ndoroboni, Kijiji cha Kiru Six, kwa tuhuma za kuunganishiwa umeme kinyume na taratibu na sheria za shirika hilo.
Afisa Uhusiano wa TANESCO Mkoa wa Manyara, Samwel Mandar, amesema operesheni hiyo ni sehemu ya msako unaoendelea wa kukagua miundombinu ya shirika, ikiwemo mita za umeme, ili kubaini wananchi wanaotumia umeme kwa njia zisizo halali.
Mandar amesema katika ukaguzi huo, wamebaini mita zinazodaiwa kuwa feki na ambazo hazionyeshi matumizi halisi ya umeme, hali ambayo inaweza kusababisha upotevu wa mapato kwa shirika.
Kwa upande wake, Msimamizi wa Kitengo cha Udhibiti Mapato TANESCO Mkoa wa Manyara, Maisha Mchuruza, amesema watuhumiwa hao walikuwa wameunganishiwa umeme bila kufuata utaratibu unaotakiwa na TANESCO.
Mchuruza amewataka wananchi kuacha mara moja kutumia njia zisizo halali kupata huduma ya umeme na badala yake kufuata taratibu rasmi za kuomba na kuunganishiwa umeme.
Baadhi ya watuhumiwa hao wamedai kuwa waliunganishiwa umeme na mtu mmoja aliyejitambulisha kuwa ni mfanyakazi wa TANESCO, ambaye aliwaomba fedha kwa ahadi ya kuwaunganishia huduma hiyo.
Wamesema walimpa fedha hizo bila kujua kuwa njia iliyotumika haikuwa utaratibu rasmi wa TANESCO.
Naye Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ndoroboni, Kijiji cha Kiru Six, Ramadhani Juma, amesema hakuwa na taarifa kuhusu wananchi hao kuunganishiwa umeme kwa utaratibu huo.
Juma amewataka wananchi katika eneo hilo kufuata hatua zote rasmi za kuomba na kuunganishiwa umeme, huku akisisitiza umuhimu wa kutoa taarifa kwa mamlaka husika endapo kuna mtu anayejitambulisha kuwa mfanyakazi wa TANESCO na kuomba fedha kwa ajili ya huduma ya umeme.
TANESCO imeendelea kuwataka wananchi kutumia njia rasmi kupata huduma za umeme na kutoa taarifa kuhusu vitendo vinavyohusisha wizi wa umeme, udanganyifu au uharibifu wa miundombinu ya shirika.

