Rais wa.chemba ya Taifa ya biashara ,Vicent Minja wakati akizungumza katika ufunguzi wa jukwaa la kushughulikia malalamiko ya walipa kodi (ombudsman) jijini Arusha.

………..
Na Happy Lazaro, Arusha.
Sekta binafsi imeitaka Serikali kuimarisha na kuiwezesha zaidi Ofisi ya Ombudsman wa Kodi kwa kuipatia wataalamu wa kutosha pamoja na bajeti inayokidhi mahitaji, ili iweze kutekeleza ipasavyo jukumu lake la kushauri Serikali na kusaidia kutatua changamoto za kikodi kabla hazijageuka kuwa migogoro.
Hayo yamesemwa jijini Arusha leo na Rais wa.chemba ya Taifa ya biashara ,Vicent Minja wakati akizungumza katika ufunguzi wa jukwaa la kushughulikia malalamiko ya walipa kodi (ombudsman) ambalo limewakutanisha wadau mbalimbali, wakiwemo wataalamu wa masuala ya kodi kutoka ndani na nje ya nchi.
Minja amesema kuwa, Ofisi ya Ombudsman wa Kodi inapaswa kuwa kiungo muhimu kati ya Serikali na wafanyabiashara kwa kusikiliza changamoto zinazowakabili walipa kodi, kuzifanyia utafiti na kuwasilisha mapendekezo kwa mamlaka husika kwa ajili ya hatua stahiki.
Akizungumza kuhusu umuhimu wa jukwaa hilo, amesema uwezeshaji wa kutosha utaifanya jukwaa hilo la Ombudsman kuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kushughulikia malalamiko ya wafanyabiashara na kutoa ushauri kwa Serikali kuhusu namna bora ya kuboresha mfumo wa kodi.
“Ni muhimu sana hii ofisi iwezeshwe, ipate wataalamu wa kutosha, lakini ipate pia bajeti ya kutosha kuhakikisha kwamba kazi ambayo imeundwa kufanya inafanyika,” amesema.
Amesema jukwaa hilo linapaswa kufanya kazi kwa karibu zaidi na sekta binafsi kwa kupokea maoni na malalamiko ya wafanyabiashara, kuyafanyia uchambuzi na utafiti, kisha kutoa mapendekezo yatakayosaidia Serikali kuchukua hatua kabla changamoto hizo hazijazalisha migogoro mikubwa ya kikodi.
“endapo mgogoro wa kikodi utatokea, Ofisi ya Ombudsman inapaswa kuwa miongoni mwa taasisi zinazosaidia kuutatua mapema, ili kupunguza muda na gharama ambazo wafanyabiashara hulazimika kutumia kufuata taratibu ndefu za mabaraza au mahakama za kodi.”amesema Minja .
Amesisitiza kuwa masuala ya kodi hayapaswi kuangaliwa kwa mtazamo wa wafanyabiashara wakubwa pekee, bali yanapaswa kuwahusisha wafanyabiashara wadogo ambao nao hukutana na changamoto mbalimbali katika shughuli zao za kila siku.
Ametolea mfano changamoto zilizowahi kujitokeza katika eneo la Kariakoo, akisema Ofisi ya Ombudsman inaweza kutumia nafasi yake kuchunguza chanzo cha changamoto hizo, kufanya utafiti na kutoa mapendekezo yatakayosaidia Serikali kuchukua hatua za kuzuia matatizo kama hayo kujitokeza tena.
Minja amefafanua kuwa, wafanyabiashara wadogo na wakubwa wanapaswa kuwa na fursa ya kufika katika Ofisi ya Ombudsman na kueleza changamoto wanazokutana nazo katika masuala ya kodi, huku ofisi hiyo ikitumia mrejesho huo katika kutoa ushauri wakati wa mchakato wa kubadili sheria, sera na viwango vya kodi.
Aidha ameomba kutungwa kwa sheria ya independence ya Tax Ombudsman na sio kuwekwa ndani ya sheria ya kodi/ TRA.
“Mfumo huo utaiwezesha Serikali kupata mrejesho wa moja kwa moja kutoka kwa sekta binafsi na kufanya maboresho yanayozingatia hali halisi ya wafanyabiashara, jambo litakalosaidia kupunguza migogoro ya kikodi na kujenga mazingira rafiki zaidi ya biashara nchini.”amesema Minja .
Sekta binafsi imeeleza kuwa kuwepo kwa Ofisi ya Ombudsman wa Kodi yenye wataalamu na rasilimali za kutosha kutasaidia kujenga uhusiano mzuri zaidi kati ya Serikali na walipa kodi, huku changamoto zikitatuliwa mapema kabla hazijawa migogoro mikubwa
