Na Sophia Kingimali, Dar es Salaam
BARAZA la Mitihani Tanzania (NECTA) limewaonya watahiniwa wa Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE) dhidi ya kujihusisha na vitendo vya udanganyifu, likisisitiza kuwa matokeo ya mtahiniwa atakayekiuka kanuni yatafutwa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 8, 2026, Katibu Mtendaji wa NECTA, Prof. Said Ally Mohamed, amesema maandalizi ya mtihani huo yamekamilika na karatasi pamoja na nyaraka muhimu za mitihani zimesambazwa katika mikoa yote ya Tanzania Bara.
Amesema watahiniwa 1,168,649 kutoka shule 20,019 wanatarajiwa kufanya mtihani huo kesho na keshokutwa, Septemba 9 na 10, 2026, huku wavulana wakiwa 531,467, sawa na asilimia 45.48, na wasichana 637,182, sawa na asilimia 54.52.
Kwa mujibu wa Prof. Mohamed, watahiniwa 1,081,204, sawa na asilimia 92.52, watafanya mtihani kwa lugha ya Kiswahili, wakati 87,445, sawa na asilimia 7.48, watafanya kwa lugha ya Kiingereza.
Amesema pia watahiniwa 4,867 wenye mahitaji maalum wamesajiliwa kufanya mtihani huo, wakiwemo wasioona 82, wenye uoni hafifu 1,551, wenye uziwi 999, wenye ulemavu wa akili 576 na wenye ulemavu wa viungo 1,659.
Amesema mtihani huo utahusisha masomo sita ambayo ni Kiswahili, English Language, Sayansi na Teknolojia, Hisabati, Maarifa ya Jamii na Stadi za Kazi, pamoja na Uraia na Maadili, huku mazingira ya vituo yakiwa yameandaliwa kwa ajili ya kuhakikisha mitihani inafanyika kwa usalama na utulivu.
Prof. Mohamed amezitaka Kamati za Mitihani za Mikoa na Halmashauri kuhakikisha usalama wa vituo unaimarishwa na mitihani inasimamiwa kwa kuzingatia Sheria, Taratibu, Kanuni na Mwongozo uliotolewa na NECTA ili kuzuia mianya ya udanganyifu.
“Baraza halitarajii kuona mtahiniwa yeyote akijihusisha na vitendo vya udanganyifu. Mtahiniwa atakayebainika kufanya udanganyifu, matokeo yake yatafutwa kwa mujibu wa Kanuni za Mitihani,” amesema.
Aidha, ameitaka jamii kushirikiana na NECTA kwa kutoa taarifa kuhusu vitendo vyovyote vinavyoweza kuhatarisha uendeshaji wa mtihani huo, ili kuhakikisha wanafunzi wanafanya mitihani kwa uadilifu, amani na utulivu.
