Waziri wa fedha Zanzibar, Dkt. Juma Malik Akil akizungumza wakati wa ufunguzi wa jukwaa la kushughulikia malalamiko ya walipa kodi (ombudsman) jijini Arusha .
Msuluhishi wa maswala ya kikodi ,Erastus Mtui akizungumza kwenye jukwaa hilo
………..
Happy Lazaro,Arusha .
Arusha.Kuimarishwa kwa mfumo wa kushughulikia malalamiko ya walipa kodi (ombudsman) kumetajwa kuwa muhimu katika kuhakikisha wanapata haki na kujenga uwazi katika ukusanyaji wa mapato nchini.
Hayo yamesemwa jijini Arusha leo na Waziri wa fedha Zanzibar, Dkt. Juma Malik Akil wakati wa ufunguzi wa jukwaa la kushughulikia malalamiko ya walipa kodi (ombudsman), limewakutanisha wadau mbalimbali, wakiwemo wataalamu wa masuala ya kodi kutoka ndani na nje ya nchi.
Dkt.Juma amesema uwepo wa mfumo imara wa kushughulikia malalamiko ya walipa kodi (ombudsman) utasaidia walipa kodi kupata suluhisho pale wanapohisi hawajatendewa haki na taasisi za kodi.
Amesema kuwa ,Jukwaa hilo kufanyika nchini Tanzania limetajwa kuwa muhimu katika kuimarisha haki, uwazi na usawa kati ya walipa kodi na taasisi zinazokusanya na kusimamia kodi.
Dkt.Juma amesema kuwa , mwaka 2024 Tanzania ilianzisha taasisi iliyo chini ya Wizara ya Fedha inayojulikana kama TOSTA, yenye jukumu la kushughulikia malalamiko ya walipa kodi dhidi ya taasisi zinazohusika na masuala ya kodi.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa baraza la Taifa la biashara, Dkt. Godwin Wanga, amesema mfumo wa kodi unapaswa kuzingatia haki kwa walipa kodi, huku akisisitiza utekelezaji wa mapendekezo ya tume ya maboresho ya kodi.
Naye Msuluhishi wa maswala ya kikodi ,Erastus Mtui amesema kuwa,Ofisi inayoshughulikia malalamiko na taarifa za kodi imefanikiwa kushughulikia jumla ya malalamiko na taarifa 593 ndani ya kipindi cha miaka miwili na nusu, huku ikieleza kuwa utatuzi wa changamoto hizo hauishii katika kushughulikia malalamiko ya mtu mmoja mmoja bali pia kuchunguza chanzo cha matatizo yanayojitokeza mara kwa mara.
Mtui amesema kuwa,amesema sheria inawapa mamlaka ya kuchambua chanzo cha malalamiko pale wanapobaini kuwa changamoto zinazowasilishwa na wananchi au wafanyabiashara zinafanana.
Amesema malalamiko yanaweza kuwasilishwa na mwananchi mmoja, mfanyabiashara au mwekezaji na kushughulikiwa moja kwa moja kwa mujibu wa taratibu, lakini pale wanapobaini malalamiko yanayofanana kujirudia, huanza kuchunguza chanzo cha tatizo hilo.
“Ukipata malalamiko moja, halafu ukapata la pili mpaka la tatu au kumi, ukaona yanafanana, unaanza kusema hapa kuna tatizo. Kwa hiyo tunaenda kuangalia tatizo ni nini na chanzo chake ni nini,” amesema Mtui.
Mtui amesema utaratibu huo ni muhimu kwa sababu unasaidia kutatua tatizo kwa upana zaidi badala ya kushughulikia malalamiko ya mtu mmoja mmoja pekee, jambo ambalo linaweza kusaidia kupunguza malalamiko yanayojirudia.
Ameongeza kuwa,uchambuzi huo unaweza kuibua aina mbili za changamoto ikiwemo zile zinazohusu utekelezaji wa masuala ya kodi ndani ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ambapo ofisi hiyo inaweza kutoa mapendekezo kwa TRA kuhusu maeneo yanayohitaji kuboreshwa au kubadilishwa.
Amesema aina ya pili ni changamoto zinazotokana na sera za kodi, ambapo baada ya kubaini chanzo cha tatizo, mapendekezo yanaweza kuwasilishwa katika Wizara ya Fedha ili yaweze kuzingatiwa katika mchakato wa kutengeneza au kuboresha sera.
Amesema njia hiyo ni muhimu katika kujenga mfumo bora wa kodi kwa sababu inasaidia mamlaka kutambua matatizo yanayojirudia na kuyafanyia kazi katika chanzo chake, badala ya kusubiri malalamiko mapya kila mara.
Mfumo huo unalenga kuhakikisha malalamiko ya walipa kodi yanasikilizwa na kutatuliwa kwa haki, hatua inayotarajiwa kuongeza uwazi, uwajibikaji na imani katika mfumo wa ukusanyaji wa mapato.

