Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi imeanza kuimarisha mbinu za kudhibiti uingizaji, usambazaji na matumizi ya dawa bandia na bidhaa nyingine zisizokidhi viwango nchini.
Akizungumza katika kikao kazi kati ya TMDA na Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa TMDA, Adam Fimbo, amesema ushirikiano huo ni muhimu katika kuhakikisha wananchi wanatumia dawa, vifaa tiba, vitendanishi na bidhaa za tumbaku zenye ubora, usalama na ufanisi.
Amesema TMDA ina jukumu la kudhibiti bidhaa hizo kuanzia hatua ya usajili, uingizaji nchini, usambazaji hadi matumizi, ili kuhakikisha zinakidhi viwango vinavyotakiwa.
“Majukumu yetu makubwa ni kuhakikisha bidhaa hizo ni bora, salama na zina ufanisi kwa matumizi ya binadamu na mifugo,” amesema.
Amesema kabla ya bidhaa kuingia nchini, lazima zisajiliwe na mamlaka hiyo baada ya kuthibitishwa kupitia tafiti na uchunguzi wa kitaalamu unaoonyesha kuwa zina ubora, usalama na ufanisi unaokubalika.
Aidha, amesema TMDA hufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maduka ya jumla na rejareja pamoja na maeneo mengine ya usambazaji, kuhakikisha bidhaa zinazouzwa ni zilizosajiliwa na kuruhusiwa kuingia sokoni.
Fimbo amesema mamlaka hiyo pia huchukua sampuli za bidhaa kutoka maeneo mbalimbali na kuzipeleka katika maabara zake kwa uchunguzi wa kitaalamu ili kubaini kama zinakidhi viwango vilivyowekwa.
Amesema maabara hizo hupokea pia sampuli zinazokamatwa na Jeshi la Polisi wakati wa operesheni na doria mbalimbali, ambapo hufanyiwa uchunguzi ili kutoa ushahidi wa kitaalamu unaoweza kutumika katika kesi mahakamani.
“Jeshi la Polisi linapokamata sampuli mbalimbali, huletwa kwetu kwa ajili ya kuthibitisha kama zinakidhi viwango vya ubora. Uchunguzi huu hutuwezesha kutoa vielelezo vinavyoweza kutumika kwenye kesi mbalimbali mahakamani,” amesema.
Ameongeza kuwa TMDA ina jukumu la kuondoa sokoni bidhaa zisizokidhi viwango na kuziteketeza katika maeneo maalumu ili kuzuia zisirejee katika soko na kuhatarisha afya za wananchi.
Vilevile, amesema TMDA hushirikiana na Polisi na taasisi nyingine za Serikali katika vituo vya mipakani kudhibiti uingizaji wa bidhaa hizo nchini na kuhakikisha zinazoingia ni zile zilizoidhinishwa.
Kikao hicho kimewakutanisha viongozi na askari wa Jeshi la Polisi kutoka maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, wakiwamo makamanda wa Polisi wa mikoa ya Temeke, Kinondoni na Ilala pamoja na wakuu wa upelelezi wa mikoa hiyo.
Fimbo amesema kikao hicho ni sehemu ya mpango wa TMDA wa kuimarisha uhusiano na Jeshi la Polisi, ambapo mamlaka hiyo imeanza kufanya vikao vya aina hiyo katika kanda zake na inatarajia kuviendesha katika mikoa mingine nchini.
“Tumekuwa tukifanya vikao kazi na waandishi wa habari katika kanda mbalimbali Tanzania, lakini hatujawahi kufanya vikao kama hivi na Polisi. Tumeona umuhimu wa kuanza utaratibu huu ili tukutane, tujenge uelewa na kujadili kwa pamoja namna ya kudhibiti bidhaa hizi,” amesema.
Amesema TMDA ina kanda nane nchini na inatarajia kufanya vikao hivyo kila mwaka kwa lengo la kuongeza uelewa wa majukumu ya kila upande na kuimarisha ushirikiano katika utekelezaji wa sheria.
Mbali na udhibiti wa bidhaa hizo, Fimbo amesema TMDA pia inasimamia majaribio ya dawa yanayofanyika kwa wanyama, pamoja na kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi salama ya dawa na bidhaa nyingine zinazodhibitiwa na mamlaka hiyo.

