Mhandisi Nuru Said (kushoto), akitoa maelezo ya mradi ya tenki la maj Sahwa kwa Waziri wa Maji Jumaa Aweso (kulia aliyekunja mikono), leo.

Mafundi wakifunga nati za moja ya bomba la mradi huo wa tenki.

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amiri Mkalipa, akizungumza na wananchi.

Kaimu Mkurugenzi a Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira wa MWAUWASA, Mhandis Leonard Msenyele, akifafanua hali ya huduma ya maji.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso,  akizungumza na waandishi wa habari wakiwemo wananchi wa Sahwa, leo.

………

NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA

SERIKALI kupitia Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, imeongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maji katika Jiji la Mwanza, hivyo hakuna sababu ya wananchi kuendelea kukabiliwa na  mgao wa maji wakati hatua mbalimbali zimechukuliwa kuongeza uzalishaji, uhifadhi na usambazaji wa huduma hiyo.

Miongoni mwa hatua hizo ni kukamilisha ujenzi wa matenki matano yenye uwezo wa kuhifadhi jumla ya lita milioni 31 za maji.

Aweso alisema hayo leo, alipokagua maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Mfumo wa Usambazaji Maji Mwanza Kusini, akisema Serikali inatambua ongezeko la watu na mahitaji makubwa ya maji jijini humo.

Hivyo, hatua nyingine ni kuendelea kuboresha vyanzo vya maji, ikiwemo Butimba, ambacho kwa sasa kina uwezo wa kuongeza zaidi ya lita milioni 48 za maji kwa siku.

Alisema kuongeza uzalishaji pekee hakutoshi bila kuwa na miundombinu madhubuti ya kuhifadhi na kusambaza maji, ndiyo maana Serikali imewekeza katika ujenzi wa matenki hayo katika maeneo ya Buhongwa, Fumagila, Kisesa, Nyamazobe na Usagara, sehemu kubwa ya ujenzi imekamilika na kilichobaki ni masuala ya kiufundi kabla ya kuanza kutumika.

Ili kuharakisha utekelezaji wa mradi huo, Aweso alimtaka Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, kuitisha kikao cha haraka kati ya mkandarasi, timu ya ufundi ya wizara na mshauri wa mradi, ili kubaini namna ya kupunguza muda wa utekelezaji, kuongeza nguvu kazi na kuhakikisha vifaa vinavyohitajika vinapatikana kwa wakati.

Alisema Serikali inaendelea na mpango wa kuongeza uzalishaji katika chanzo cha Capripoint, ambacho kwa sasa kina uwezo wa kuzalisha lita milioni 90 kwa siku. Alisema mradi huo unaotekelezwa na SUMA JKT kwa gharama ya zaidi ya Sh bilioni 22, utaongeza uzalishaji hadi lita milioni 144 kwa siku.

Alisema ongezeko hilo litasaidia kupunguza changamoto ya maji katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Mwanza, ikiwemo Buswelu, Kahama, Kiseke na Kishiri, akisisitiza kuwa Serikali haitaki maji yanayozalishwa yabaki kwenye vyanzo, bali yawafikie wananchi.

Aweso alisema Serikali ilifanya mabadiliko ya kiutendaji katika Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) baada ya kubaini changamoto mbalimbali, ikiwemo uzembe wa baadhi ya watumishi na mapungufu katika ukusanyaji wa mapato.

Alisema hatua hizo zimeanza kuleta matokeo, ambapo zaidi ya wananchi 2,000 waliokuwa wamelipia kuunganishiwa huduma ya maji bila kupata huduma hiyo sasa wameunganishiwa.

Aidha, alisema zaidi ya Sh milioni 700 ambazo awali hazikuonekana katika mapato ya taasisi zimepatikana, hatua iliyowezesha MWAUWASA kulipa mishahara ya watumishi na kuendelea na shughuli nyingine za uendeshaji.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amiri Mkalipa, alisema mabadiliko ya menejimenti ya MWAUWASA yaliyofanyika yameanza kuleta matokeo, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono hatua hizo.

“MWAUWASA ni Idara ya Serikali, changamoto zake pia ni za Serikali. Kazi yetu ni kuwahudumia wananchi. Wezi wa maji watashughulikiwa, wakiwemo watumishi wanaoshirikiana nao; safari yao imefika mwisho, wabadilike,” alisema.

Mkalipa aliiagiza Idara ya Uhusiano na Habari ya MWAUWASA kuwaeleza wananchi kuhusu ongezeko la mapato na mabadiliko ya menejimenti, huku akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuisimamia taasisi hiyo.

Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira wa MWAUWASA, Mhandisi Leonard Msenyele, alisema mahitaji ya maji jijini Mwanza ni makubwa kuliko uwezo wa uzalishaji wa vyanzo vilivyopo.

Alisema matenki ya Buhongwa na Fumagila yana uwezo wa kuhifadhi lita milioni 10 kila moja, Kisesa na Nyamazobe lita milioni tano kila moja, na Usagara lita milioni moja, huku mradi huo ukihusisha pia ujenzi wa kituo cha kusukuma maji cha Sahwa na kugharimu takribani Sh bilioni 46.2.

Mhandisi Msenyele alisema Serikali inaendelea na awamu ya pili ya upanuzi wa chanzo cha Butimba, ambapo uzalishaji utaongezeka kutoka lita milioni 48 hadi milioni 70 kwa siku, sambamba na kuongeza uwezo wa Capripoint kutoka lita milioni 90 hadi milioni 144 kwa siku.

Naye Mbunge wa Ilemela, Kafiti Kafiti, alisema ujenzi wa matenki hayo umefikia asilimia 80, akisema yeye na Mbunge wa Nyamagana, John Nzilanyingi, wanaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha changamoto ya maji katika majimbo hayo inamalizika na kuwa historia.