Mkuu wa Idara ya Biashara wa Benki ya Stanbic Tanzania, Fredrick Max (kushoto), na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar, ZEEA, Juma Burhan Mohamed (kulia), wakionesha nakala za Hati ya Makubaliano ya miaka mitano inayolenga kuimarisha ujasiriamali, upatikanaji wa huduma za kifedha na ukuaji endelevu wa biashara Zanzibar. Utiaji saini huo ulishuhudiwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdullah, wakati wa Maonyesho ya Fahari ya Zanzibar 2026.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, akishuhudia utiaji saini wa Hati ya Makubaliano ya miaka mitano kati ya Benki ya Stanbic Tanzania na Taasisi ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar, ZEEA, yenye lengo la kuimarisha ujasiriamali, upatikanaji wa huduma za kifedha na ukuaji endelevu wa biashara Zanzibar. Makubaliano hayo yalisainiwa na Mkuu wa Idara ya Biashara wa Benki ya Stanbic Tanzania, Fredrick Max (kushoto), pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa ZEEA, Juma Burhan Mohamed (kulia0, wakati wa Maonyesho ya Fahari ya Zanzibar 2026.
…………..
Makubaliano haya yatapanua msaada kwa wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo na wa kati walioko Unguja na Pemba.
Ushirikiano huu unaimarisha jukumu kuu la ZEEA la uwezeshaji wananchi kiuchumi na utaalamu wa kifedha ulioko Stanbic, uendelezaji wa biashara na uunganishaji wa wafanyabiashara na masoko tofauti.
Utiaji saini huo unafanyika katika Maonyesho ya Fahari ya Zanzibar 2026, ambapo benki ya Stanbic ndiye mdhamini mkuu kwa kuwezesha jumla ya Shilingi milioni 200.
Zanzibar, Tanzania – Jumamosi, tarehe 5 Septemba 2026: Benki ya Stanbic Tanzania na Taasisi ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA) leo zimesaini Hati ya Makubaliano ya miaka mitano ya kuanzisha ushirikiano wa kimkakati wa kuimarisha ujasiriamali, upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wote na ukuaji endelevu wa biashara Zanzibar.
Makubaliano hayo yalisainiwa wakati wa uzinduzi rasmi wa Maonyesho ya Fahari ya Zanzibar 2026 katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, na kushuhudiwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdullah.
Kiini cha ushirikiano huu ni nia ya pamoja ya kuzisaidia biashara nyingi zaidi za Zanzibar kutoka katika hatua ya uwezo uliopo na kufikia ukuaji endelevu. Stanbic na ZEEA zitashirikiana kuimarisha elimu ya fedha, urasimishaji wa biashara, upatikanaji wa mitaji, huduma za kifedha za kidijitali, uendelezaji wa biashara pamoja na upatikanaji wa masoko kwa wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo na wa kati katika Unguja na Pemba.
Ushirikiano huu unajengwa juu ya lengo la Fahari ya Zanzibar yenyewe. Maonyesho haya ya kitaifa ya biashara yalianzishwa ili kuvipatia bidhaa na biashara za Zanzibar nafasi ya kufika sokoni, kwa kuwaunganisha wajasiriamali na wateja, wanunuzi, taasisi za fedha, wawekezaji pamoja na wadau wa uendelezaji wa biashara. Mwaka huu maonyesho yanatarajiwa kuwavutia zaidi ya wageni 15,000 na waonyeshaji zaidi ya 300 kutoka sekta mbalimbali zikiwemo kilimo, uvuvi, utalii, ubunifu, viwanda, usindikaji wa vyakula na uchumi wa ubunifu.
Kwa upande wa Stanbic, ushirikiano huu unaakisi mtazamo mpana wa mahitaji halisi ya biashara ili ziweze kufanikiwa. Upatikanaji wa mitaji bado ni jambo la muhimu, lakini ukuaji endelevu pia unategemea uwezo imara wa kuendesha biashara, usimamizi mzuri wa fedha, utayari wa kidijitali, upatikanaji wa masoko, ushauri elekezi pamoja na mitandao sahihi ya kibiashara.
Fredrick Max, Mkuu wa Idara ya Biashara Stanbic Bank, amesema makubaliano haya yanaipa Benki na ZEEA jukwaa muhimu la kuwasaidia wajasiriamali wengi zaidi kugeuza ndoto zao kuwa biashara zenye tija na ushindani. “Zanzibar haikosi wajasiriamali, mawazo, wala dhamira. Fursa iliyopo sasa ni kuzisaidia biashara nyingi zaidi kuugeuza uwezo huo kuwa ukuaji wa kweli. Jambo hilo linahitaji mitaji, lakini pia linahitaji maarifa, mifumo imara ya biashara, uwezo wa kidijitali, masoko na mahusiano. Ushirikiano wetu na ZEEA unaviunganisha vipengele hivi vyote ili wajasiriamali wengi zaidi waweze kujenga biashara zilizo tayari kukua.”
Makubaliano haya pia yatafungua fursa kwa wajasiriamali wanaokidhi vigezo kuunganishwa na programu za Stanbic za uendelezaji wa biashara, ikiwemo Stanbic Biashara Incubator pale inapohusika. Programu hiyo huwapa wajasiriamali msaada wa kivitendo katika kuendeleza biashara, ushauri elekezi, nyenzo na mitandao inayolenga kuimarisha uwezo wa biashara na utayari wa kukua.
Katika kipindi chote cha Fahari ya Zanzibar, timu ya Stanbic Biashara Incubator itakuwepo katika viwanja vya maonyesho ikiwahudumia wajasiriamali na kutoa msaada wa kivitendo kwa wafanyabiashara. Timu nyingine za Stanbic pia zitakutana na wafanyabiashara kuzungumzia suluhisho za biashara ya kimataifa, biashara ya kilimo, miamala ya kidijitali pamoja na mikopo ya magari na mitambo.
Stanbic imetoa udhamini wa Shilingi milioni 200 kwa Maonyesho ya Fahari ya Zanzibar 2026 kama Mdhamini wa Ngazi ya Platinamu. Benki inauona uwekezaji huu kama sehemu ya dhamira pana kwa biashara na wajasiriamali watakaoiongoza Zanzibar katika hatua yake ijayo ya ukuaji wa kiuchumi. “Udhamini wetu wa Shilingi milioni 200 si jambo la udhamini pekee. Ni ishara ya imani tuliyo nayo kwa wajasiriamali wa Zanzibar, bidhaa zao na uwezo wa kiuchumi wa visiwa hivi,” amesema Max.
Ushirikiano huu unakuja mwaka mmoja tangu Stanbic ifungue huduma zake Zanzibar, jambo linaloashiria hatua mpya kutoka kuwepo tu na kuelekea kujenga mahusiano ya kina na wananchi na biashara zinazoendesha uchumi wa visiwa.
“Mwaka mmoja tangu tuanze safari yetu hapa, tuko wazi kuhusu nafasi tunayotaka kuichukua. Zanzibar ni nyumbani kwetu, na tunaendelea kuchochea ukuaji wake. Kuiita Zanzibar nyumbani maana yake ni kuwekeza kwa watu wake, biashara zake na uwezo wake wa kiuchumi wa muda mrefu. Tunataka kuzisaidia biashara ziwe imara hapa nyumbani, na kuziunganisha zile zenye dhamira na uwezo na fursa zilizopo Tanzania, Afrika na masoko ya kimataifa,” ameongeza Max.
Juma Burhan Mohamed, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA), amesema ushirikiano huu utaimarisha juhudi za kuwaunganisha wajasiriamali na msaada wanaouhitaji ili kujenga biashara endelevu. “Uwezeshaji wa kiuchumi unahitaji ushirikiano unaowapa wajasiriamali njia za kivitendo za kukua. Kupitia ushirikiano huu, ZEEA na Stanbic zitaunganisha uendelezaji wa biashara, uwezo wa kifedha, upatikanaji wa huduma stahiki za kifedha pamoja na uunganishaji na masoko ili kuwasaidia wajasiriamali wa Unguja na Pemba. Lengo letu ni kutengeneza fursa zinazozaa biashara imara na thamani ya kiuchumi ya kudumu kwa Zanzibar.”
Chini ya Hati hii ya Makubaliano, Stanbic na ZEEA zitaandaa programu mbalimbali zitakazokubaliwa zenye kuunga mkono ujasiriamali, uendelezaji wa biashara ndogo na za kati, upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wote, upatikanaji wa mitaji, urasimishaji wa biashara na uunganishaji na masoko. Ushirikiano huu pia utafungua fursa za makongamano ya kibiashara, maonyesho, mafunzo ya kujenga uwezo pamoja na mipango mingine ya uendelezaji wa biashara.
Mafanikio ya ushirikiano huu hatimaye hayatapimwa kwa makubaliano yaliyosainiwa katika Fahari ya Zanzibar pekee. Thamani yake itaonekana katika wajasiriamali imara zaidi, biashara nyingi zaidi zilizo tayari kupata mikopo, bidhaa nyingi zaidi za Zanzibar kufika sokoni, na biashara nyingi zaidi zinazotengeneza ajira na kuchangia ukuaji endelevu wa uchumi wa visiwa hivi.
