Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imepongeza Halmashauri ya Chalinze kwa kutumia mapato ya ndani kuwekeza katika miradi ya kimkakati yenye lengo la kuongeza mapato, ajira na kuboresha huduma kwa wananchi.
Pongezi hizo zimetolewa Septemba 06, 2026 na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Florent Kyombo, wakati Kamati ilipofanya ziara ya kukagua miradi minne katika Halmashauri ya Chalinze mkoani Pwani, ikiwemo uwanja wa michezo, Hospitali ya Wilaya, Stendi ya Mabasi na mradi wa kibiashara wa Kituo cha Mafuta.
Mhe. Kyombo amesema Kamati imeridhishwa na uwekezaji huo, akieleza kuwa Halmashauri imetumia zaidi ya Shilingi Bilioni 5.7 za mapato ya ndani katika ujenzi wa uwanja wa michezo, huku Serikali ikiwekeza zaidi ya Shilingi Bilioni 1.4 katika ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Chalinze.
Aidha, amesema Halmashauri imewekeza Shilingi Milioni 925 za mapato ya ndani katika ujenzi wa mradi wa kibiashara wa kituo cha mafuta, ambacho pamoja na miradi mingine ya kimkakati kinatarajiwa kuongeza vyanzo vya mapato na kuchochea shughuli za kiuchumi katika Halmashauri hiyo.
Hata hivyo, Kamati imetoa angalizo kuhusu matumizi ya Stendi ya Mabasi ya Chalinze, baada ya kubaini baadhi ya mabasi kushusha na kupakia abiria nje ya eneo rasmi la stendi, licha ya Serikali kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu hiyo.
Mhe. Kyombo ameitaka Halmashauri kwa kushirikiana na Mkuu wa Wilaya ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, Baraza la Madiwani na Mkurugenzi, kuhakikisha sheria na mipango miji inasimamiwa ili mabasi yote yashushe na kupakia abiria ndani ya stendi, jambo litakalosaidia kuongeza usalama na kipato kwa wafanyabiashara.
Kwa upande mwingine, Mwenyekiti huyo ameitaka Halmashauri kuhakikisha miradi yote inakamilishwa kwa wakati kwa mujibu wa mikataba ili ianze kutoa manufaa yaliyokusudiwa, huku akiipongeza Serikali ya Mkoa, Wilaya na Halmashauri ya Chalinze kwa ushirikiano unaochangia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

