Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Dodoma

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Prof. Palamagamba Kabudi, amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuzindua majengo ya ofisi za wizara 26, taasisi za Serikali 11 pamoja na barabara za lami zenye urefu wa kilomita 57.1 katika Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma, Septemba 8, 2026. Akizungumza Septemba 6, 2026 jijini Dodoma na waandishi wa habari, Prof. Kabudi amesema uzinduzi huo utafanyika katika Uwanja wa Mashujaa na utahusisha pia miundombinu ya maji safi na majitaka, umeme, taa za barabarani na mawasiliano.Amebainisha kuwa awamu ya kwanza ya ujenzi wa Mji wa Serikali ilihusisha majengo 23 ya ofisi za awali yaliyojengwa kuanzia Novemba 28, 2018 hadi Machi 22, 2019, huku awamu ya pili ya ujenzi wa majengo ya kudumu ilianza Oktoba 2021.

Aidha, ameongeza kuwa awamu ya pili imehusisha pia ujenzi wa barabara za lami zenye urefu wa kilomita 57.1, huku miundombinu ya umeme yenye urefu wa kilomita 42 ikiwekwa chini ya ardhi pamoja na mifumo ya maji safi na majitaka.Kuhusu gharama, Prof. Kabudi amesema awamu ya pili ya ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba ilipangwa kutumia Shilingi bilioni 940, huku hadi sasa Shilingi bilioni 698 zikiwa zimetumika katika ujenzi.

Amesema Serikali imewekeza fedha kwa ajili ya ujenzi na ukamilishaji wa Mji wa Serikali Mtumba, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa uamuzi wa kuhamisha makao makuu ya nchi kwenda Dodoma uliofanyika mwaka 1973.

Amebainisha kuwa ujenzi huo umehusisha kwa kiasi kikubwa wakandarasi na taasisi za ndani, ambapo majengo ya wizara na taasisi yamejengwa na wakandarasi 11, kati yao watano wakiwa taasisi za Serikali na sita kutoka sekta binafsi.Aidha, amesema miundombinu mbalimbali imetekelezwa na taasisi za Serikali zikiwemo TARURA, DUWASA, TANESCO, TTCL, TEMESA, eGA, TPDC, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na TFS.

Prof. Kabudi amesema Mji wa Serikali umejengwa kwa kuzingatia dhana ya Smart City, ikiwemo mji wa kijani, matumizi ya nishati mbadala, uvunaji wa maji ya mvua na matumizi ya teknolojia katika uendeshaji wa huduma.

Ameongeza kuwa majengo hayo yana uwezo wa kuhudumia watumishi 18,510, huku barabara hizo zikiimarisha usafirishaji na upatikanaji wa huduma ndani na nje ya Mji wa Serikali.

Pia ametoa wito Kwa  wananchi wa Dodoma na maeneo ya jirani kujitokeza kwa wingi kushuhudia uzinduzi huo. Huku akibainisha Kuwa amesema na fataki katika eneo la Mtumba Center saa 6 usiku wa kuamkia Septemba 8, 2026, kuashiria tukio hilo