Na Mwandishi wetu – Kilimanjaro

Septemba 03, 2026 Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Siha imefungua na kushinda shauri la jinai Na. 19847/2026 ikiwa ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania dhidi ya Bw. Oscar Timotheo Kiwale aliyekuwa Meneja wa Mradi wa Maji Magadini Makiwaru. Shauri hilo limesikilizwa katika Mahakama ya Wilaya ya Siha mbele ya Mhe. Elibahati Petro – Hakimu Mkazi Mfawidhi na limeendeshwa na Mwendesha Mashtaka wa Serikali Bw. Bernard Ndamallya.

Bw. Oscar ameshtakiwa kwa kosa la kupokea hongo chini ya kifungu cha 15 (1) (a) (2) na (3) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 Marejeo ya mwaka 2023. Akiieleza Mahakama Bw. Ndamallya alisema kuwa Hospitali ya Charlotte iliunganisha maji kinyemela na baada ya ukaguzi kufanyika hospitali hiyo ilitakiwa kulipa faini kiasi cha Tsh. 5,000,000/= kwa kosa hilo.

Mnamo Aprili 09, 2026 mshtakiwa alipokea fedha kiasi cha Tsh. 900,000/= kutoka kwa Mhasibu wa Hospitali ya Charlotte ili asitoze faini iliyostahili kulipwa.

Mnamo Septemba 03, 2026 mtuhumiwa alifikishwa mahakamani na alikiri kosa, hivyo Mahakama ilimtia hatiani na kumhukumu kulipa faini ya Tsh. 500,000/= au kutumika kufungo cha miaka mitatu gerezani. Vilevile Mahakama ilitoa amri kwa mshtakiwa kulipa Tsh. 900,000 kwa mhanga ambaye ni Magadini Makiwaru Water Supply Trust ndani ya siku saba kuanzia tarehe ya hukumu. 

Mshtakiwa alitekeleza kulipa malipo ya faini zote kama ilivyoelekezwa na Mahakama siku hiyohiyo ya hukumu na aliachiwa huru.