Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) Septemba 5, 2026 imeongeza nguvu katika ulinzi na usimamizi wa rasilimali za wanyamapori baada ya askari wapya 268 kuhitimu mafunzo ya kijeshi katika Chuo cha Mafunzo ya Jeshi la Uhifadhi Mlele, mkoani Katavi.

Askari hao wamehitimu baada ya kukamilisha mafunzo ya miezi sita yaliyowajengea uwezo katika maeneo mbalimbali, ikiwemo matumizi sahihi ya silaha, mfumo wa taarifa za kijiografia (GIS), utimamu wa mwili, nidhamu, haki za binadamu, udhibiti wa wanyamapori wakali na waharibifu pamoja na maadili ya kijeshi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Mhe. Majid Mwanga, amesema Serikali imeendelea kuimarisha Jeshi la Uhifadhi kwa kuongeza nguvu kazi na kuboresha miundombinu mafunzoni.

“ Nendeni mkafanye kazi kwa nidhamu, uadilifu, uwajibikaji, uzalendo, bidii, weledi na ubunifu sawa na viapo vyenu bila upendeleo wala rushwa ili muweze kuwa misingi muhimu ya Jeshi la Uhifadhi lenye ufanisi. “ 

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya TAWA, Prof. Jafari Kidegesho ameishukuru Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha TAWA kuongeza nguvu kazi, vitendea kazi na kuboresha mazingira ya mafunzo kwa ajili ya kuimarisha uhifadhi.

Naye, Kaimu Kamishna wa Uhifadhi, Mlage Yussuf Kabange amesema kuwa uwezeshaji unaotolewa na Serikali umeendelea kuimarisha shughuli za uhifadhi na utalii. TAWA inajukumu la kuhakikisha rasilimali za wanyamapori na maliasili zinalindwa kikamilifu ili ziendelee kuwa msingi wa shughuli za utalii, uwekezaji na maendeleo ya wananchi.

“ Askari 268 wanatarajiwa kuongeza nguvu katika ulinzi wa rasilimali za wanyamapori, kukabiliana na ujangili, kuimarisha usalama katika maeneo ya hifadhi na kuchangia juhudi za Serikali za kukuza sekta ya utalii na uwekezaji nchini “.

Kamishna Kabange amewataka askari hao wapya kuwa mstari wa mbele katika kudhibiti ujangili, kulinda mazingira na rasilimali za Taifa, huku akisisitiza umuhimu wa kushirikiana na jamii kwa kutoa elimu ya uhifadhi na kupunguza migogoro kati ya binadamu na wanyamapori ili kuendelea kulinda rasilimali za Taifa “.