Mwamvua Mwinyi, Kibaha

Septemba 6, 2026

MJUMBE wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Pwani, Alhaj Mussa Mansoor, amekabidhi vifaa vyote vya ujenzi wa ofisi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Mkuza, Kibaha Mjini, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kujenga na kuimarisha chama hicho.

Aidha, Mansoor amewezesha vikundi mbalimbali katika kata hiyo kwa jumla ya Sh milioni 3.5, ambapo Tawi la Wakereketwa Bodaboda Backyard limepatiwa Sh 500,000, wajane Sh 500,000, watu wenye ulemavu Sh 500,000, wajasiriamali Sh 500,000, wacheza draft Sh 500,000, huku wazee wakipatiwa Sh milioni moja.

Akizungumza na wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa CCM Kata ya Mkuza, Mansoor ameahidi kuwezesha fedha kwa ajili ya mradi wa mtaji wa waendesha bodaboda, pamoja na kutoa vizibao na banda la chuma litakalotumika kama ofisi ya umoja wa waendesha bodaboda baada ya uongozi wa umoja huo kuwasilisha changamoto hiyo.

Vilevile, amemuelekeza Katibu wa CCM kata, Ofisa Maendeleo ya Jamii kata na Diwani wa kata hiyo kumpatia vikundi vya wanawake wajasiriamali ili aweze kuvipatia fedha za kuwawezesha katika shughuli zao za kiuchumi.

Mansoor pia anaendelea na taratibu za kuwawezesha Bima ya afya wazee wa kata hiyo hatua ambayo itasaidia kupata huduma ya afya kwa urahisi.

“Nawashukuru wananchi kwa kuichagua CCM kuanzia ngazi ya Rais, Mbunge na madiwani, kwa sasa kipindi cha uchaguzi kimekwisha, uchaguzi usitugawe, Ikumbukwe kila kiongozi aliyechaguliwa ana nafasi ya kukijenga chama, tushirikiane, tuwe na umoja pasipo chuki tukijenge chama,” alisisitiza Mansoor.

Katika hatua nyingine, Mansoor ametoa viti 100 kwa ajili ya mradi wa UVCCM Kata ya Kongowe, baada ya awali kukabidhi fedha Sh milioni 2.5 kwa ajili ya mradi huo, ambazo hata hivyo zilitumika tofauti na lengo alilokusudia.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Kata ya Mkuza, Matata Ngolo, amemshukuru Mansoor kwa kuwaunga mkono katika ujenzi wa ofisi ya chama kwa kutoa vifaa vyote, pamoja na kuwezesha vikundi mbalimbali.

Mwenyekiti wa Makada Mkoa wa Pwani, Khamis Mponji maarufu Wayne, amesema Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anahitaji viongozi wanaokipenda na kukijenga chama, hivyo makada wataendelea kuwaunga mkono viongozi wanaotekeleza wajibu huo.

Naye Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Kibaha Mjini, Ramadhani Kazembe, amesema viongozi na wanachama wanaokilinda na kukijenga chama wanapaswa kuungwa mkono, huku akisisitiza kuwa kila mwanachama na kiongozi ana wajibu wa kukiimarisha CCM.

Ameshauri vijana kukitumikia chama kwa kuzingatia umoja na kuepuka kujiingiza katika migogoro inayoweza kujitokeza miongoni mwa wanasiasa.