Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Tanzania iko tayari kuimarisha zaidi ushirikiano na Serbia katika biashara na uwekezaji, kilimo, utalii, elimu na Uchumi wa Buluu, ili uhusiano wa muda mrefu baina ya nchi hizo mbili uendelee kuleta matokeo ya kiuchumi yenye manufaa kwa wananchi.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 02 Septemba 2026, jijini Belgrade, Serbia, alipokutana na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Serbia, Mhe. Prof. Đuro Macut, akiwa pamoja na ujumbe wake.
Amesema ziara yake nchini Serbia imefungua fursa mpya za kuendeleza ushirikiano wa kiuchumi, akieleza kuwa mazungumzo yaliyofanyika na viongozi wa Serikali pamoja na wafanyabiashara na wawekezaji wa Serbia yameonesha kuwepo kwa maeneo mbalimbali yanayoweza kuendelezwa kwa manufaa ya pande zote.
Katika sekta ya kilimo, Rais Dkt. Mwinyi amesema Tanzania ina nia ya kushirikiana na Serbia katika upatikanaji wa mbolea, mbegu, teknolojia za kilimo na uchakataji wa mazao, akibainisha kuwa kilimo kina nafasi kubwa katika uchumi wa Tanzania na kinatoa fursa pana za uwekezaji na uongezaji thamani.
Aidha, amesema Tanzania ina fursa kubwa katika sekta ya utalii, ikiwemo vivutio maarufu duniani vya Mlima Kilimanjaro, Serengeti na Ngorongoro pamoja na Zanzibar, hivyo kuwepo kwa safari za ndege za moja kwa moja kati ya Serbia na Tanzania kutasaidia kuongeza idadi ya watalii, biashara na uwekezaji baina ya nchi hizo mbili.
Kwa upande wa Uchumi wa Buluu, Rais Dkt. Mwinyi amesema Zanzibar ina fursa kubwa katika uvuvi, uzalishaji wa mwani na shughuli nyingine za baharini, huku akieleza umuhimu wa kutafuta masoko zaidi ya bidhaa hizo nchini Serbia na katika mataifa mengine ya Ulaya.
Rais Dkt. Mwinyi pia amepongeza hatua ya Serbia ya kufungua Ubalozi wake wa kudumu nchini Tanzania, akieleza kuwa Serikali ya Tanzania tayari imetenga eneo katika Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma, kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi za Ubalozi pamoja na makaazi ya Balozi wa Serbia.
Kuhusu elimu, Rais Dkt. Mwinyi ameishukuru Serikali ya Serbia kwa kutoa fursa za ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa Tanzania, akieleza kuwa fursa hizo zinaweza kusaidia kuongeza utaalamu katika maeneo mbalimbali, hususan kilimo na sekta nyingine za maendeleo.
Dkt. Mwinyi pia amemfikishia Waziri Mkuu Macut salamu kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kuishukuru Serikali na wananchi wa Serbia kwa mapokezi na ukarimu waliouonesha kwa ujumbe wa Tanzania wakati wa ziara hiyo.
Aidha, ameipongeza Serikali ya Serbia kwa maandalizi mazuri ya Mkutano Maalum wa Ngazi ya Juu wa Kumbukumbu ya Miaka 65 tangu kufanyika kwa Mkutano wa Kwanza wa Wakuu wa Nchi wa Harakati za Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM), uliofanyika jijini Belgrade.
Naye, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Serbia, Mhe. Prof. Đuro Macut, ameeleza kufurahishwa na ziara ya Rais Dkt. Mwinyi nchini humo, akisema inaendeleza urafiki wa kihistoria kati ya Tanzania na Serbia uliojengwa tangu enzi za Yugoslavia. Amesema Serbia inathamini mchango wa Tanzania katika kuendeleza uhusiano huo wa muda mrefu.
Amesema misingi ya harakati za NAM bado una umuhimu mkubwa katika mazingira ya sasa ya dunia, hususan katika kuhimiza ushirikiano wa mataifa bila masharti au migawanyiko ya kisiasa. Ameongeza kuwa Tanzania ina nafasi muhimu katika historia ya Harakati hiyo.
Prof. Macut amesema bado kuna fursa kubwa za kupanua mahusiano ya kiuchumi kati ya nchi hizo mbili, akitaja biashara, utalii, kilimo na uchakataji wa mazao, uzalishaji wa mbegu na mbolea pamoja na sekta ya uvuvi. Aidha, amesema kuimarika kwa mahusiano hayo kutafungua njia ya kuanzishwa kwa usafiri wa anga wa moja kwa moja kati ya Tanzania na Serbia.
Akizungumzia kuitangaza Tanzania nchini Serbia, Waziri Mkuu huyo ameeleza matumaini yake kuwa Tanzania itatumia EXPO 2027 kutangaza vivutio vyake vya utalii, fursa za uwekezaji na uwezo wake wa kiuchumi kwa wafanyabiashara na wananchi wa Serbia.
Kabla ya kuhitimisha ziara yake nchini humo, Rais Dkt. Mwinyi ametembelea Makumbusho ya Yugoslavia, katika eneo la Nyumba ya Maua (House of Flowers) jijini Belgrade, ambako amejionea kumbukumbu za aliyekuwa Rais wa Yugoslavia, Josip Broz Tito, na mchango wake katika historia ya NAM. Tito amezikwa katika eneo hilo, ambapo Rais Dkt. Mwinyi pia ameweka shada la maua katika kaburi lake ikiwa ni ishara ya heshima.
Rais Dkt. Mwinyi anatarajiwa kuondoka nchini Serbia leo, tarehe 02 Septemba 2026, kurejea Zanzibar baada ya kukamilisha ziara yake iliyojumuisha kushiriki Mkutano wa NAM, pamoja na shughuli mbalimbali za kidiplomasia, kihistoria na kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Serbia.

