Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imeendelea kuwaalika wamiliki wa viwanda na waajiri nchini Tanzania kwa ajili ya kushirikiana katika kuendeleza kwa wananchi.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa VETA CPA Anthony Kasore leo tarehe 4 Septemba, 2026 wakati wa kutiliana saini Hati ya Makubaliano (MoU) na kampuni ya Van Mo ya jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kushirikiana katika kuendeleza ujuzi kwa vijana na kuwawezesha kuajirika mara moja baada ya kuhitimu mafunzo yao.
Makubaliano hayo yamesainiwa na pande mbili katika ukumbi wa mikiutano wa VETA Makao Makuu jijini Dodoma, yakihusisha CPA Anthony Kasore, Mkurugenzi Mkuu wa VETA na Meneja Mkuu wa Kampuni ya Van Mo, Fathi Ahmed Ally. Kampuni ya Van Mo inajishughulisha na usafirishaji, uchukuzi, biashara za uuzaji mafuta, miliki (majengo na ardhi), kilimo, utalii, na shughuli zingine za uzalishaji viwandani.
Malengo ya MoU iliyosainiwa ni pamoja na kukuza upatikanaji wa wahitimu wenye umahiri, tija, ubunifu, maadili na wanaozingatia usalama kazini, Van Mo kutoa fursa za ajira kwa wahitimu wa VETA wenye sifa zinazostahili, kuoanisha programu za mafunzo ya ufundi stadi na mahitaji katika sekta ya viwanda na biashara pamoja na kuwezesha mafunzo kwa vitendo katika maeneo ya kazi.
MoU iliyosainiwa inayataja maeneo mahsusi ya ushirikiano kuwa ni mafunzo ya udereva wa magari makubwa, na usimamizi wa vyombo vya usafiri, uchukuzi na uhifadhi wa mizigo pamoja na usimamizi wa mnyororo wa ugavi, ukaguzi wa magari ukarabati, mifumo ya umeme na elektroniki ya magari, uendeshaji wa maghala na usimamizi wa stoo, uendeshaji wa vituo vya mafuta, ujenzi, usimamizi wa majengo na miundombinu sambamba na uendeshaji wa shughuli za utalii na ukarimu na kilimo na uhifadhi wa mazao.
Akizungumza mara baada ya kusainiwa kwa makubaliano hayo, Mkurugenzi Mkuu wa VETA CPA. Anthony Kasore amesema makubaliano hayo yanalenga kuwajengea uwezo wakufunzi na kuongeza kuwa VETA itaendelea kuwa na ushirikiano na waajiri na wamiliki wa viwanda ili kuhakikisha kinachofundishwa kinaendana na mahitaji halisi ya soko la ajira hivyo kuawezesha wahitimu wa VETA kuajirika katika viwanda na maeneo mengine lakini pia kushirikiana nao ili kutambua fursa zilizopo.
“Tutahakikisha pia wenzetu wa VAN MO wanapohitaji wataalamu wenye ujuzi mbalimbali sisi VETA tuweze kusaidia kawapata sambamba na hilo ushirikiano huu una maslahi mapana kwaaajili ya wananchi kuweza kupata fursa za ajira” amesema Kasore.
Kwa upande wake Meneja Mkuu wa Kampuni ya VAN MO Fathi Ahmed Ally amesema wamelenga kuwapatia ajira vijana takribani 500 wenye ujuzi mbalimbali ambao wamehitimu katika vyuo vya VETA.
“Kilichotuvutia kuja VETA ni kutokana na wahitimu kutoka katika vyuo hivi kuwa na ujuzi ambao sisi tunauhitaji katika kampuni yetu hususan shughuli za usafirishaji hivyo tumeona hapa ndipo mahali sahihi pa kuwapata hao vijana wenye ujuzi huo” amesema Fathi.

