Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni akiwasilisha maelezo kuhusu azimio la kuridhia Mkataba wa Uanzishwaji wa Taasisi ya Ukuzaji wa Maendeleo ya Kijani Duniani, bungeni jijini Dodoma leo Septemba 03, 2026.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Reuben Kwagilwa (kulia) akishiriki kikao cha Bunge jijini Dodoma leo Septemba 03, 2026. Wengine ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. James Milya na Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Mshamu Munde 

Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Maduhu Kazi (katika) akifuatilia kikao cha Bunge jijini Dodoma leo Septemba 03, 2026. Katika kikao hicho Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni aliwasilisha maelezo kuhusu Azimio la kuridhia Mkataba wa Uanzishwaji wa Taasisi ya Ukuzaji wa Maendeleo ya Kijani Duniani. Wengine pichani ni Wakurugenzi Wasaidizi Idara ya Mazingira Dkt. Paul Deogratius (kushoto) na Dkt. Kanizio Manyika.

…………

Bunge limeridhia azimio la kuridhia Mkataba wa Uanzishwaji wa Taasisi ya Ukuzaji wa Maendeleo ya Kijani Duniani (GGGI) lililowasilishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni bungeni jijini Dodoma leo Septemba 03, 2026.

Kupitia Mkataba huo Tanzania itapata manufaa yakiwemo kuongeza uwezo wake katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kukuza uchumi unaolenga kuzingatia hifadhi ya mazingira.

Awali akiwasilisha maelezo hayo, alisema Taasisi ya kimataifa ya ikilenga kushirikiana na nchi wanachama katika uandaaji wa miradi ya uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi; kusaidia taasisi za ndani za nchi wanachama kupata ithibati katika usimamizi wa fedha za Mifuko.

GGGCI upatikanaji wa fedha za misaada na mikopo yenye riba nafuu kwa nchi pamoja na uwekezaji kwenye hati fungani za kijani utaongezeka na hivyo kuchochea mazingira endelevu kwa ustawi wa nchi.

“Mheshimiwa Spika endapo tutairidhia azimio hili nchi yetu itakuwa na ongezeko la taasisi zenye ithibati katika usimamizi wa fedha za mifuko ya kimataifa ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi na kuongezeka kwa wigo wa kidiplomasia na ushawishi wa nchi katika medani za kisiasa, kiuchumi na uhifadhi wa mazingira,“ alisema.

Pamoja na faida za kuridhiwa mkataba huo, Mhe. Mhandisi alieleza kuwa umelenga kuimarisha upatikanaji wa nishati safi na maji safi kwa gharama nafuu kupitia ushirikiano kati ya nchi zilizoendelea kwa kusaidia na kuwezesha dhana ya ukuaji wa uchumi wa kijani.

Halikadhalika, alibainisha kuwa mkataba huo utachagiza jitihada za Serikali za hifadhi endelevu ya mazingira ikiwemo upunguzaji wa uzalishaji wa gesijoto na uhimilivu mabadiliko ya tabianchi.

Akitoa maoni kuhusu azimio hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira Mhe. Jackson Kiswaga alishauri kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais ipewe jukumu la kuratibu shughuli zote zinazohusiana na GGGI, kwa kuwa mkataba huo unahusisha utekelezaji kupitia sekta mbalimbali hususani uchumi, mazingira, mabadiliko ya tabianchi, uwekezaji, nishati, kilimo, maji, viwanda na maendeleo ya jamii.

Pia, alishauri kuwa Serikali baada ya kujiunga na Taasisi ya GGGI, ifanyetathimini ya mara kwa mara juu ya mabadiliko ya Sheria yanayoweza kufanyika baada ya kujiunga ili yasiathiri utekelezaji wa miradi ya kimkakati na vipaumbele vya Kitaifa.

Mhe. Kiswaga ambaye pia ni mbunge wa Kalenga alisema ni muhimu baada ya kujiunga na GGGI, Serikali ifanye tathimini ya jumla ili kuona kama matarajio ya malengo yamefikiwa.

Halikadhalika, alishauri Serikali iisimamie taasisi hiyo ili iweze kushirikiana na Wataalam wa ndani ya Nchi, kwa ajili ya kutoa msaada wa kitaalaam katika kuandaa maandiko ya miradi ya kijani nchini.

Wakichangia azimio hilo, baadhi ya wabunge wameunga mkono na kusisitiza kuwa litakuwa na manufaa makubwa katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na usimamizi endelevu wa mazingira.

Mbunge wa Buhingwe Mhe. Prof. Pius Yanda alisema taasisi hiyo itakayoanzishwa itakuwa ni nyenzo mojawapo ya kusaidia katika utekelezaji wa malengo chini ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

“Tumeona nchi wanachama zikiwemo za Afrika Mashariki zimeanza kufaidika kwa hivyo ni muhuimu tuwe na utayari wa kuandaa mapendekezo kuona namna ya kushirikiana hatua itakayosaidia kupata fedha,“ alisema.

Pia, Prof. Yanda ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira alisema inahitajika teknolojia ya ziada katika masuala mazima ya hifadhi ya mazingira.

Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalumu Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana alishauri Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC) kutumia wataalamu wake kutoa elimu ya biashara ya kaboni kwa wananchi wanaoshi katika maeneo yenye misitu.