Raia wa Oman, Mohammed Abdallah Al-Habsy na familia yake wakiangalia chumba chenye mashine ya Linear Accelerator (LINAC) kinachotumika kutoa matibabu ya saratani kwa tiba ya mionzi kwa wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI).

Raia wa Oman, Mohammed Abdallah Al-Habsy pamoja na familia yake wakizungumza na kumfariji mgonjwa wakati akipatiwa tiba ya kemia katika wodi maalumu ya kutolea huduma hiyo katika Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI).

Raia wa Oman, Mohammed Abdallah Al-Habsy akisaini kitabu cha wageni wakati wa ziara yake ya kujionea huduma za matibabu ya Saratani zinazotolewa katika Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) iliyopo jijini Dar es Salaam

Raia wa Oman, Mohammed Abdallah Al-Habsy akiwa katika picha ya pamoja na familia yake na Daktari Bingwa wa Tiba Nyuklia wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) Tausi Maftah mara baada ya kumaliza ziara yake ya kutembelea ORCI kwaajili ya kuona huduma za matibabu ya Saratani zinazotolewa.

Mtaalamu wa Tiba ya Mionzi wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) Fredrick Ludovick akimweleza Raia wa Oman, Mohammed Abdallah Al-Habsya jinsi huduma za matibabu ya mionzi zinavyotolewa kwa wagonjwa wanaotibiwa katika taasisi hiyo wakati wa ziara yake ya kujionea huduma za matibabu ya Saratani zinavyotolewa ORCI.

Mtaalamu wa Tiba ya Mionzi wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) Fredrick Ludovick akimwononesha Raia wa Oman, Mohammed Abdallah Al-Habsya moja ya chumba kilichofungwa mashine mpya ya Cobalt ambayo ufungwaji wake ukikamilika itatumika kutoa huduma ya tiba ya mionzi kwa wagonjwa wa Saratani.
………………..
Na Mwandishi Maalumu – Dar es Salaam
Raia wa Oman, Mohammed Abdallah Al-Habsy ameipongeza Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) kwa uwekezaji mkubwa katika teknolojia na vifaa tiba vya kisasa, miundombinu pamoja na mazingira rafiki kwa wagonjwa huku akisema alichokiona katika Taasisi hiyo kinaonesha hatua kubwa iliyopigwa na Tanzania katika utoaji wa huduma za matibabu ya saratani.
Pongezi hizo amezitoa hizi karibuni baada ya Al-Habsy pamoja na familia yake kutembelea ORCI walipokuwa nchini Tanzania kwa mapumziko ambapo walipata fursa ya kujionea kwa karibu huduma, miundombinu na teknolojia mbalimbali zinazotumika katika utambuzi na matibabu ya saratani.
Al-Habsy alisema kwa muda mrefu wamekuwa wakisikia kuhusu ORCI na kuvutiwa na huduma zinazotolewa na Taasisi hiyo hivyo basi walipopata fursa ya kufika Dar es Salaam waliamua kutembelea ORCI ili kujionea wenyewe mazingira na huduma zinazotolewa.
Alisema ziara hiyo imempa fursa ya kuelewa kwa karibu namna huduma za matibabu ya saratani zinavyotolewa nchini Tanzania pamoja na kuona uwekezaji uliofanyika katika vifaa tiba na miundombinu ya kisasa.
“Nimevutiwa na mazingira, miundombinu, vifaa tiba vya kisasa pamoja na huduma zinazotolewa na ORCI, huduma za matibabu ya saratani alizoziona zinafanana kwa kiwango kikubwa na huduma zinazotolewa nchini Oman, taasisi hii ina mambo mengi ambayo Tanzania inaweza kujivunia kimataifa”.
“Ziara hii imenipa mtazamo chanya kuhusu huduma za saratani zinazotolewa nchini Tanzania na ninaahidi kuwa balozi wa ORCI kwa kuzungumzia huduma na maendeleo niliyoyaona kwa watu wengine nchini Oman pamoja na wadau mbalimbali. Nitaendelea kuzungumzia nilichokiona hapa na kuwaeleza wengine kuhusu huduma na teknolojia nilizoziona Ocean Road”, alisema Al-Habsy.
Kwa upande wake Tausi Maftah ambaye ni Daktari Bingwa wa Tiba Nyuklia wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) alisema uwepo wa wageni kutoka nje ya Tanzania katika taasisi hiyo ni fursa muhimu ya kukuza utalii tiba kwa kuwa wageni wanapofika na kujionea wenyewe ubora wa huduma, miundombinu na teknolojia zinazotumika katika matibabu ya saratani wanaweza kufikisha taarifa hizo katika jamii zao na kusaidia kujenga uaminifu kuhusu huduma zinazopatikana nchini.
Dkt. Tausi alisema ziara hiyo pia ni sehemu ya juhudi za kuitangaza Tanzania kama eneo linaloweza kutoa huduma za matibabu ya saratani kwa wagonjwa kutoka ndani na nje ya nchi kutokana na uwepo wa wataalamu wenye ujuzi, vifaa tiba vya kisasa na miundombinu inayowezesha utoaji wa huduma za kibingwa za saratani.
Aliongeza kuwa wageni kama Al-Habsy na familia yake wanapotembelea ORCI na kushuhudia huduma zinazotolewa wanakuwa sehemu muhimu ya kueneza taarifa sahihi kuhusu uwezo wa Tanzania katika sekta ya afya.
“Taarifa walizoziona hapa zinaweza kusaidia kujenga uelewa na imani kwa jamii za kimataifa kuhusu huduma za matibabu ya saratani zinazopatikana nchini jambo ambalo litasaidia kuongezeka kwa wagonjwa kutoka mataifa mbalimbali wanaokuja Tanzania kwa ajili ya matibabu”.
Kuimarika kwa utalii tiba kuna manufaa kwa uchumi wa nchi kwani wagonjwa na wageni wanaokuja kwaajili ya matibabu hutumia huduma nyingine kama usafiri malazi na shughuli za utalii”, alisema Dkt. Tausi.
Ziara hiyo inaendelea kuonesha umuhimu wa uwekezaji katika teknolojia, vifaa tiba na miundombinu ya kisasa katika kuimarisha huduma za saratani nchini huku ORCI ikiendelea kutoa huduma za kibingwa kwa wagonjwa kutoka Tanzania na nje ya nchi.
