Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Jacob John Mkunda Akizungumza katika hafla ya maadhimisho ya miaka 62 tangu kuanzishwa kwa (JWTZ) iliyofanyika Septemba 1, 2026 Viwanja vya Gofu vya Lugalo jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Wiki ya Sita ya Ushirikiano wa Majeshi ya Afrika Mashariki 2026, Brigedia Jenerali Dkt. Agatha Mary Katua, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Utawala wa JWTZ, akieleza. mambo kadhaa katika hafla hiyo. 

………….

Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limeadhimisha miaka 62 tangu kuanzishwa kwake tarehe 1 Septemba 1964, katika hafla iliyofanyika Septemba 1, 2026 katika Viwanja vya Gofu vya Lugalo jijini Dar es Salaam, huku maadhimisho hayo yakiambatana na kufungwa rasmi kwa Wiki ya Sita ya Ushirikiano wa Kijeshi na Kiraia wa Majeshi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Jacob John Mkunda, amesema JWTZ limeendelea kuwa nguzo muhimu katika kulinda uhuru, amani na usalama wa Tanzania, pamoja na kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo na huduma kwa wananchi.

Jenerali Mkunda amesema maadhimisho hayo yana umuhimu wa pekee kwa kuwa yanaunganisha historia ya miaka 62 ya JWTZ na juhudi za kuimarisha ushirikiano baina ya majeshi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika masuala ya kijeshi na kiraia.

Amesema katika kipindi cha miaka 62, JWTZ limeendelea kujenga uwezo, weledi na uzalendo miongoni mwa wanajeshi wake, huku likitekeleza majukumu yake ya msingi ya kulinda mipaka, Katiba na maslahi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Wiki ya Sita ya Ushirikiano wa Majeshi ya Afrika Mashariki 2026, Brigedia Jenerali Dkt. Agatha Mary Katua, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Utawala wa JWTZ, amesema wiki hiyo imekuwa fursa muhimu ya kuimarisha ushirikiano na mshikamano wa majeshi ya nchi wanachama.

Brigedia Jenerali Dkt. Katua amesema katika kipindi cha wiki hiyo, timu za pamoja kutoka Burundi, Kenya, Rwanda, Uganda, Somalia na Tanzania zilifanya kazi bega kwa bega katika kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi wa Dar es Salaam, Pwani pamoja na Zanzibar.

Amesema jumla ya wananchi 11,749 walipatiwa huduma za matibabu bila malipo katika vituo saba vya afya, vikiwemo Hospitali ya Mbweni, Hospitali ya Vingunguti, Hospitali ya Tumbi na Hospitali ya Bagamoyo.

Aidha, Brigedia Jenerali Dkt. Katua amesema washiriki walitoa misaada kwa vituo vya kulea watoto yatima, watu wenye mahitaji maalumu, makazi ya wazee na taasisi nyingine za kijamii, huku wakifanya ukarabati na maboresho ya miundombinu katika baadhi ya vituo vilivyofikiwa.

Amesema shughuli hizo zimeonesha kwa vitendo maana ya kaulimbiu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki isemayo “Watu Wamoja, Hatima Moja,” kwa kuwa zimewawezesha wanajeshi kutoka nchi wanachama kufanya kazi pamoja na kuwahudumia wananchi.

Brigedia Jenerali Dkt. Katua amesema Wiki ya Ushirikiano wa Kijeshi na Kiraia ilitokana na mapendekezo ya Kikundi Kazi cha Wataalamu wa Ulinzi katika Michezo na Utamaduni kilichokutana mwaka 2016 na kuweka mapendekezo pamoja na taratibu za utekelezaji wa shughuli hizo.

Amesema dhamira ya wiki hiyo ni kuwaleta karibu zaidi askari wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, kuimarisha ushirikiano wao na kutumia uwezo na utaalamu wao kuwahudumia wananchi na kuchangia maendeleo ya jamii.

Brigedia Jenerali Dkt. Katua pia ameeleza kuwa kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luteni Jenerali Salum Haji Othman, kwa ajili ya kuzindua wiki hiyo, kamati ilikuwa imeandaa shughuli mbalimbali za kuhakikisha utekelezaji wa programu unafanyika kwa ufanisi.

Amezishukuru nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kushiriki katika shughuli hizo, akisema wataalamu waliotumwa wamewezesha kubadilishana uzoefu na maarifa, hususan katika eneo la huduma za afya na huduma za kijamii.

Amesema JWTZ litaendelea kushirikiana na majeshi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika shughuli za kijeshi na kiraia, huku likiboresha mipango na utekelezaji wa shughuli hizo ili ziwe na manufaa makubwa zaidi kwa wananchi na kuimarisha mshikamano wa kikanda.