Na Sophia Kingimali, Dar es Salaam

Chuo cha Ufundi FURAHIKA (VETA) Education College kimetangaza nafasi 250 za mafunzo kwa vijana wa Kiislamu, huku kikieleza kuwa nafasi hizo zitatolewa kwa ajili ya kuwawezesha vijana kupata ujuzi wa ufundi na fani mbalimbali kwa gharama nafuu.

Akizungumza na wanahabari Leo Septemba 1,2026 jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Chuo hicho, Dkt. David Msuya, alisema chuo hicho kinaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhakikisha vijana wanapata elimu na ujuzi badala ya kubaki mitaani.

“Chuo kimetoa nafasi 250 kwa vijana wa Kiislamu, wakiwemo wanafunzi wanaoletwa na Jumuiya ya Waislamu na BAKWATA, ambapo wanafunzi hao watapata nafasi ya kusoma kwa utaratibu maalumu na kuchangia zaidi gharama za mitihani pekee”.Amesema Msuya.

Dkt. Msuya alisema fursa hizo zinahusisha fani mbalimbali, ikiwemo udereva, TEHAMA, malezi ya watoto, umeme wa majumbani, useremala, utengenezaji wa sofa, ushonaji, urembo, upishi na utengenezaji wa keki, pamoja na kozi za hoteli na huduma za ndege na viwanja vya ndege.

Aidha Dkt. Msuya ameongeza kuwa vijana wanaweza kujiunga na kozi mbalimbali zikiwemo za muda wa mwaka mmoja, miaka miwili na kozi fupi za miezi sita, huku akisisitiza kuwa baadhi ya mafunzo yanatolewa bure na mwanafunzi kuchangia gharama za mitihani pekee.

Alisema nafasi hizo pia zitatolewa kwa vijana wanaomaliza darasa la saba na kidato cha nne, ambapo watapata fursa ya kujifunza TEHAMA, udereva, malezi ya watoto, ushonaji, umeme wa majumbani, useremala, utengenezaji wa sofa, mapambo ya keki, saluni na fani nyingine za kuwawezesha kujiajiri.

Dkt. Msuya pia aliwataka wazazi kutoka mikoa mbalimbali nchini kuwapeleka watoto wao chuoni hapo, akisema chuo kina hosteli na mazingira mazuri ya kujifunzia, pamoja na mafunzo ya lugha za Kichina, Kifaransa na Kiingereza yanayotolewa sambamba na fani nyingine.

Katika hatua nyingine, alisema chuo hicho kimeendelea kuwakaribisha vijana wenye ulemavu na mahitaji maalum, isipokuwa wale wasioona kutokana na kukosekana kwa mwalimu mwenye utaalamu wa lugha inayohitajika, huku akisisitiza kuwa lengo ni kuhakikisha vijana wanapata ujuzi na baadaye wanaingia katika soko la ajira.

Sambamba na hayo Dkt. Msuya alisema chuo hicho kimeongeza muda wa kupokea wanafunzi hadi Septemba 20, 2026, huku akiwataka wazazi, vijana, taasisi na mashirika mbalimbali kutumia fursa hiyo. Alisema pia chuo kinatarajia kufanya mahafali Jumamosi wiki hii kwa kuwaaga wanafunzi 240, wakiwemo 200 wanaofadhiliwa kupitia Mfuko wa Jimbo la Ukonga na 40 wanaojisomesha wenyewe.