Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Dodoma
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), Mhe. Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya, amesema taasisi hiyo imeweka mfumo wa kuweka miadi kwa njia ya mtandao kupitia QR Code, unaolenga kupunguza msongamano wa wagonjwa katika hospitali.
Akizungumza na waandishi wa habari Septemba 1, 2026 Jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa mwaka wa fedha 2025/26 na mwelekeo wa 2026/27, Dkt. Ulisubisya amesema mgonjwa akitumia QR Code hiyo ataweza kupata taarifa kuhusu taasisi, madaktari waliopo na huduma zinazotolewa akiwa nyumbani.
Amebainisha kuwa mgonjwa ataweza kuchagua daktari anayehitaji kumuona pamoja na muda wa kufika hospitalini, huku mfumo huo ukimpatia control number ambayo ataitumia kufanya malipo kabla ya kufika.
Aidha, amesema Kuwa baada ya mgonjwa kuweka miadi, mfumo wa MOI utaonyesha taarifa za mgonjwa, daktari anayetarajiwa kumuona pamoja na kliniki na muda wa huduma, hivyo kupunguza muda wa kusubiri hospitalini.
Huku akibainisha Kuwa mfumo huo umeanzishwa kutokana na changamoto ya msongamano, ambapo kihistoria wagonjwa walikuwa wakifika hospitalini saa 10 za alfajiri na kusubiri hadi saa 8 mchana ili kuonana na daktari.
Pia, ameseme kuwa mfumo huo utawawezesha wagonjwa kufika katika muda waliopangiwa na kuendelea na shughuli nyingine, badala ya kutumia muda mrefu kusubiri huduma hospitalini.
Aidha, amesema katika mwaka wa fedha 2025/26 MOI imehudumia jumla ya wagonjwa 211,389, wakiwemo 202,000 waliokuja kupata huduma bila kulazwa na takribani 10,000 waliolazwa.
Ameongeza kuwa MOI imeendelea kuboresha huduma za mifupa na mfumo wa fahamu kwa kutumia teknolojia za kisasa, huku sasa ikikidhi asilimia 98 ya mahitaji ya wagonjwa wa mifupa, misuli na majeraha na asilimia 97 ya wagonjwa wa mfumo wa fahamu.
Aidha, MOI imeendelea kuboresha tiba ya kiharusi kwa kutumia Biplane Angiography (Cath Lab), huduma za kubadilisha nyonga na magoti, upasuaji wa magoti kwa kutumia matundu pamoja na huduma za maumivu sugu.
Ameongeza kuwa katika mwaka 2025,2026 idara ya radiolojia ilifanya vipimo takribani 84,000, huku kitengo cha physiotherapia kikihudumia wagonjwa 72,000, ikiwa ni sehemu ya juhudi za taasisi hiyo kuendelea kuboresha huduma kwa wagonjwa.
